NAIROBI, Kenya
MAKALA haya yanaanzia kwa kijana raia wa Kenya, Amon Kipruto, ambaye anavua shati na kuonesha kovu katika tumbo lake, alama aliyobaki nayo baada ya kutolewa figo aliyouza na kujipatia fedha alizoamini zingetosha kumpa utajiri.
Kipruto mwenye umri wa miaka 22, anakiri kuwa yeye ni miongoni mwa vijana wengi wa Kenya walioingia mkenge wa biashara haramu ya uuzaji wa figo zinazosafirshwa kwenda Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya.
Lakini, anasema anajutia uamuzi huo na hata kutamani asingejaribu kufanya kile alichokiamini kuwa ni sahihi miaka kadhaa iliyopita. “Natamani muda ungerudi nyuma ili nisikubali figo yangu kutolewa. Nachukia kwa kile nilichokifanya,” anasema.
Akionesha kujutia zaidi, Kipruto anasema wakati huo alidhani kuuza figo kungebadilisha maisha yake. “Nilidhani ningekuwa tajiri na kuishi vizuri.
Hata hivyo, nini angefanya kukabiliana na ugumu wa maisha? Anasema maisha ya kijijini kwao, Magharibi mwa Kenya, yalikuwa magumu, hasa baada ya ujio wa ugonjwa wa Uviko (Covid-19).
“Hali ya maisha ilikuwa mbaya. Nilipambana kutafuta kazi lakini ujira niliokuwa nalipwa kwa kuosha magari au ujezi haukutosha kumudu gharama za maisha,” anasimulia.
“Siku moja, rafiki yangu akanipa njia rahisi na ya haraka ya kuingiza Dola 6,000. Aliniambia kuuza figo kungenipa fedha nzuri. Ilikuwa ni kama bahati kuzisikia taarifa hizo.”
Mbaya zaidi kwake, hata baada ya upasuaji na kutolewa figo, Kipruto hakupewa kiasi cha fedha alichoahidiwa, na badala yake aliambulia Dola 4,000. “Niliishia kununua simu na gari, ambayo navyo viliharibika,” anasema.
Miezi michache tu baadaye, Kipruto akiwa hajapewa elimu yoyote juu ya athari zinazoweza kujitokeza akiwa na figo moja (badala ya mbili kama inavyopaswa), anasema afya yake ilianza kudhohofika na wakati mwingine kupoteza fahamu.
Kutokana na kukithiri kwa biashara hiyo ya figo, uchunguzi wa vyombo vya habari vya Ujerumani uliibuka na ripoti inayotosha kushangaza. Vyombo vilivyoshirikiana katika utafiti ni Der Spiegel, ZDF na DW.
Utafiti wao uliohusisha nyaraka na mahojiano na wadau mbalimbali, wakiwamo madaktari, ulibaini kuwa mnyororo wa biashara hiyo unahusisha pia baadhi ya hospitali za Kenya, ambazo huuza figo nchini Ujerumani.
Ikumbukwe, kwa Ujerumani, wagonjwa zaidi ya 10,000 wanakabiliwa na changamoto ya uhitaji wa figo. Tegemeo pekee ni kwa figo za maiti, ambazo hata hivyo bado hazitoshi kuhudumia idadi hiyo ya wagonjwa. Hiyo inasababisha mgonjwa anayehitaji kupandikiziwa figo kusubiri hadi miaka 10.
Sasa, aliyewahi kuwa muajiriwa wa Hospitali ya Mediheal, ambaye hata hivyo hakutaka jina lake litajwe hadharani, anasema taasisi hiyo ya Kenya ilianza biashara ya kuuza figo nchini Ujerumani miaka mingi iliyopita.
“Awali, wanunuaji walitoka Somalia. Kuanzia mwaka 2024, wanunuaji walianza kuja kutoka Israel na Ujerumani. Pia, wapo wanaotokea Azerbaijan, Kazakhstan na Pakistan,” anasema.
Kama hiyo haitoshi, Kipruto anasema zoezi la upasuaji wa kutolewa figo lilifanyika katika Hospitali hiyo iliyoko mjini Eldoret, Magharibi mwa Kenya. “Walionifanyia upasuaji ni madaktari wa India na walinipa mkataba uliokuwa umeandikwa kwa Kiingereza, lugha ambayo siielewi,” anasema.
Mwaka 2023, Wizara ya Afya ya Kenya iliagiza uchunguzi dhidi ya Hospitali hiyo na ndipo ilipobaini kuwa waliokuwa wakichangia figo hawakuwa na uhusiano wowote na wale waliowapa. Kwamba ilikuwa ni biashara.
Licha ya kubaini hilo, hakuna hatua iliyochukuliwa, ikielezwa kuwa hiyo ilitokana na nguvu aliyonayo mmiliki wa Hospitali hiyo, Swarup Mishra, ambaye ni Mbunge wa zamani na rafiki mkubwa wa Rais William Ruto.
Ilishitua zaidi kwamba licha ya skendo hiyo, bado Rais Ruto alimteua Mishra kuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Kinga ya Kenya BioVax na kuiwakilisha nchi katika Mkutano wa Shirika la Afya la Kimataifa (WHO).
Kwa upande wake, mtafiti Willis Okumu, ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Security Studies jijini Nairobi, anakiri kuzungumza na vijana wengi walioingia kwenye mtego wa biashara hiyo haramu ya kuuza figo.
Wengi wao walimwambia kuwa wanauza figo zao mjini Oyugis, eneo lililoko umbali wa kilometa 180 kutoka Eldoret. “Kwa kweli, huu ni Uhalifu mkubwa,” anasema Okumu na kusisitiza kuwa si chini ya vijana 100 wa eneo hilo wameshauza figo zao.
DW ilipofanya mahojiano na vijana wanne wa Oyugis, walisema waliuza figo zao kwa fedha kiduchu (Dola 200), kabla ya kubaini kuwa Hospitali waliyotumia iliahidiwa Dola 400 kwa kila kijana.
Okumu anaamini ni wakati sahihi sasa kwa mamlaka kutunga sheria kali dhidi ya biashara hiyo. “Kwa sasa, hakuna sheria inayokuzuia kutoa figo yako na kuuza. Huwezi kushitakiwa kokote pale,” anasema.
Published:


