13.9 C
New York

PSG v CHELSEA; Fainali ya historia Kombe la Dunia

Published:

NEW JERSEY, Marekani

JUMAPILI ya wiki hii, PSG watashuka dimbani kumenyana na Chelsea katika fainali ya kukata na shoka ya Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu.

Ni mchezo wa mwisho baada ya mwezi mmoja wa michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Mashindano hayo yalikuwa na mengi ya kushangaza, kubwa ikiwa ni Manchester City na Inter Milan kuondoshwa na Al Hilal na Fluminense, timu ambazo hazikuwa zikipewa nafasi kubwa.

PSG

Matajiri hao wa soka la Ufaransa ni tishio kwenye mashindano hayo yanayofanyika katika ardhi ya Marekani.
Kwa mujibu wa takwimu kuelekea mechi yao na Chelsea, PSG wameshinda michezo saba kati ya nane waliyoshuka dimbani hivi karibuni.

Vijana hao wa kocha Luis Enrique walionesha ‘ukatili’ wao walipoibamiza Real Madrid mabao 4-0 katika mchezo uliopita wa nusu fainali. Ikumbukwe, mabao mawili kati ya hayo yalipatikana ndani ya dakika tisa tu.
Kabla ya kukutana na Madrid, waliifungashia virago Bayern Munich kwa kichapo cha mabao 2-0.

Jeuri ya PSG katika eneo la kiungo inatokana na ubora wa Vitinha, huku pia mashambulizi ya timu hiyo yakitegemea pia makali ya mabeki wake wa pembeni, Nuno Mendes na Achraf Hakimi. Pia, uzoefu mkubwa wa kocha Enrique, ambaye amewahi kuinoa Barcelona, unaipa jeuri PSG.

CHELSEA

Blues wanafukuzia taji lao kubwa la pili ndani ya miezi ya hivi karibuni. Mwezi uliopita, walibeba ubingwa wa Conference League. Usajili mpya wa kocha Enzo Maresca, Joao Pedro, ni kama umeanza kulipa.
Ndiyo, Mbrazil huyo alicheka na nyavu mara mbili katika mchezo uliopita wa nusu fainali dhidi ya timu yake ya zamani, Fluminense.

Kwa muda mfupi, Pedro ameweza kutengeneza ‘pacha’ hatari ya ushambuliaji akiwa na Cole Palmer, pia wakisaidiwa na safu ya kiungo yenye Enzo Fernandez, Romeo Lavia na Moises Caicedo.

REKODI

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ni mwaka 2016, hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo PSG ilishinda mechi zote mbili (nyumbani na ugenini) kwa ushindi wa mabao 2-1.
Kwa mechi nane za hivi karibuni, PSG imeshinda tatu, imefungwa mbili na sare tatu.

Wakati huo huo, PSG wanajivunia rekodi ya kocha wao, Enrique, ambaye hajawahi kupoteza fainali. Mhispania huyo ameshinda mara zote 11 alizoingia hatua hiyo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img