Na Hassan Mwasha, Gazetini
SIMBA haijapata ushindi katika mechi mbili za hatua ya makundi msimu huu wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika. Kwa ufupi, iko mkiani mwa Kundi D. Baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Petro de Luanda ya Angola katika mchezo wa nyumbani, ‘Wekundu wa Msimbazi’ walikutana na kisiki kingine ikiwa ugenini dhidi ya Stade Malien ya Mali. Ikafungwa mabao 2-1.
Ni Simba ambayo msimu uliopita ilikaribia kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, kama si kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Nini kimeikuta Simba ya msimu huu, ambayo si tu haipati matokeo, bali pia inacheza soka lisilovutia ndani ya uwanja? Makala haya yanachambua. Kama ilivyo desturi ya mchezo wa soka, lawama zimeelekezwa kwa kocha Dimitar Pantev, ambaye taari ametimuliwa. Wapo wenye hoja kuwa Simba ilikurupuka kumpa ajira kocha huyo. Wanataka afukuzwe.
Sawa. Lakini, hiyo haiondoshwi ukweli kwamba lipo tatizo kubwa katika uongozi wa klabu ya Simba. Kuna shida inayopaswa kupatiwa ufumbuzi. Kabla ya mchezo dhidi ya Stade Malien, Simba ilifanya Mkutano Mkuu. Kupitia mkusanyiko huo, ungeweza kuona bila kificho ukubwa wa tatizo lililopo nje ya uwanja.
Kwa muda wote wa Mkutano huo, kama kuna jambo lililoonekana wazi, basi ni kukosekana kwa umoja ndani ya klabu. Ni rahisi kusema kuna mpasuko na makundi. Hata katika mazungumzo yake, mara kadhaa Mwenyekiti Murtaza Mangungu alishindwa kuficha hilo. Kauli zake za ‘najua kuna watu wana shida na mimi’ zilitosha kuthibitisha kuwa kuna shida.
Wakati fulani, zilisikika kauli kutoka kwa wanachama, ambazo hazikuwa za kupinga hoja, bali zilizobeba viashiria vya jeuri na chuki dhidi ya viongozi, akiwamo Mwenyekiti wao, Mangungu.
Ilifikia wakati, katika kile unachoweza kusema ni kuzidiwa na presha, Mangungu alimjibu mmoja ya wanachama akimwambia ‘kama una shida na mimi, subiri Uchaguzi’. Hii ilikuwa ni kauli ya kuthibitisha kwamba kuna shida.
Lazima viongozi wa Simba wakiri kuwa kuna shida inayopaswa kufanyiwa kazi. Kuna nyufa zimeanza kujitokeza katika jengo la umoja na mshikamano ndani ya klabu. Katika mazingira haya, ni ngumu kuiona timu ikifanya vizuri ndani ya uwanja. Ni ngumu kuona saikolojia ya wachezaji ikiwa na utimamu wa asilimia 100.
Wakati mwingine, mivutano ya aina hii huenda ikaliondoshea utulivu hata benchi la ufundi katika kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake kwenye timu. Kama hiyo haitoshi, ni rahisi mivutano ya aina hii kuruhusu wapinzani (wa ndani na nje) kupitisha ajenda zao za kuivuruga zaidi mipango ya klabu.
Hivyo basi, ni lazima viongozi wajiulize, wajitafakari, na kisha waje na suluhisho. Walikague na kulifanyia ukarabati jengo lao la umoja na mshikamano.


