MUNICH, Ujerumani
TANGU aliyojiunga na Bayern Munich akitokea Tottenham, mshambuliaji wa kimataifa wa England, Harry Kane, amefungia timu hiyo tangu Bundesliga jumla ya mabao 109 na ‘asisti’ 29 katika mechi 114.
Mkataba wake na vigogo hao wa Bundesliga utafikia ukomo mwaka 2027 lakini tayari ameanza kuhusishwa na klabu mbalimbali za nje ya Ujerumani.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari, Kane ataondoka Bayern baada ya kumalizika kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani.
Barcelona
Kama ataondoka Bayern kama inavyoripotiwa, basi huenda Kane akatimkia Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) kujiunga na Barcelona, ambayo inatajwa kuitaka saini yake.
Barcelona iko mawindoni ikisaka mshambuliaji wa kati wa kuziba pengo la Robert Lewandowski anayehusishwa na mpango wa kuondoka klabuni hapo.
Tottenham
Mwanzoni mwa mwezi huu, mtandao maarufu wa soka wa TeamTalk uliripoti kuwa Tottenham Ina mpango wa kumrejesha nahodha wake huyo wa zamani.
Hata hivyo, kwa Kane kushawishika kurudi, ni lazima klabu hiyo iwe imekata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Manchester United
Kama itakumbukwa, Kane amekuwa akihusishwa na klabu hiyo kwa miaka mingi, hata kabla ya kujiunga na Bayern mwaka 2023.
Kwa sasa, kocha wa Man United, Ruben Amorim, amekiri kuwa anahitaji straika kutokana na majeraha ya straika aliyemtoa RB Leipzig, Benjamin Sesko.
Newcastle United
Klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England nayo inahusishwa na saini ya mpachikaji mabao huyo. Kane atakwenda kuvunja rekodi ya Alan Shearer, ambaye ndiye mfungaji bora wa muda wote klabuni hapo?
Kane amewahi kuizungumzia Newcastle United akiitaja kuwa ni moja ya klabu bora kwa sasa na inayoweza kumshawishi mchezaji yeyote kujiunga nayo.
Manchester City
Kane amewahi kukaribia kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England. Ilikuwa wakati wa usajili wa kiangazi, 2023, ingawa alitimkia Bayern.
Hata hivyo, ni ngumu kuona dili hilo likifanyika kwa sasa, ikizingatiwa kuwa mkataba wa Erling Haaland utafikia ukomo mwaka 2034.
Chelsea
Kwa mujibu wa mkongwe wa Chelsea, Glen Johnson, huu ni wakati sahihi kwa Kane kuelekea Stamford Bridge.
“Nafikri kama Harry Kane yuko tayari kurudi England, basi sehemu sahihi zaidi ni Chelsea. Wamekuwa wakihitaji mchezaji wa aina hiyo,” alisema Johnson.
PSG
Kama ilivyo kwa Barcelona, Tottenham, Manchester City na Manchester United, matajiri wa Ligue 1, PSG, nao wametajwa kuimezea mate saini ya nyota huyo.
Licha ya ubora wao, bado PSG wanakosa mshambuliaji wa kati wa kiwango cha Kane, hivyo wanataka kuona wanaziba pengo hilo.
Published:


