MERSEYSIDE, England
LIVERPOOL imepoteza mechi sita kati ya saba za Ligi Kuu ya England (EPL) ilizocheza hivi karibuni. Mwenendo huo umeibua presha kubwa kwa kocha Arne Slot na huenda akatimuliwa.
Baada ya kunyakua ubingwa wa EPL msimu uliopita, safari hii mambo yamekuwa magumu kwa Liverpool, licha ya kuwa ndiyo klabu iliyotumia fedha nyingi zaidi katika usajili uliopita.
Je, ni nani kuchukua mikoba endapo mabosi wa Liverpool watachoka na kuamua kumfuta kazi kocha huyo wa kimataifa wa Uholanzi? Makala haya yanachambua.
Jurgen Klopp
Aliondoka Anfield mwaka jana akiwa na heshima kubwa. Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 58, amekiri kuwa ni moja ya ndoto zake kurudi Liverpool katika siku za usoni.
“Nilishasema sitowahi kufundisha klabu nyingine ya England. Kama itatokea (kurudi England), basi ni Liverpool,” alisema.
Oliver Glasner
Amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa. Glasner amefanya kazi kubwa akiwa Crystal Palace na ameshinda mechi zote tatu alizokutana na Slot katika siku za hivi karibuni.
Kati ya mechi hizo ni ile ya fainali ya Ngao ya Hisani ya mwanzoni mwa msimu huu. Kocha huyo aliwahi kuwindwa na klabu za Chelsea na Manchester United.
Andoni Iraola
Bournemouth ni moja ya timu zinazocheza soka la kuvutia, pia ikizipa wakati mgumu timu kubwa za Ligi Kuu ya England. Ni kutokana na uwepo wa Iraola kwenye benchi.
Kocha huyo amekuwa akitajwa kwenye rada za Manchester City, ikielezwa kuwa mabosi wa klabu hiyo wanataka atue Etihad endapo Pep Guardiola ataondoka.
Unai Emery
Akiwa na mechi zaidi ya 1,000, Mhispania huyo ni miongoni mwa makocha wenye uzoefu mkubwa. Aliwahi kupita Arsenal, Villarreal, Valencia na Sevilla.
Kwa sasa, Emery ndiye anayeipa jeuri Aston Villa. Ni kocha aliyewahi kutwaa mataji saba akiwa na vigogo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), PSG.
Julien Nagelsmann
Mjerumani huyo aliwahi kuhusishwa na Liverpool baada ya Klopp kuondoka. Hata hivyo, biashara haikufanyika, na badala yake ni Slot ndiye aliyepewa mikoba hiyo.
Nagelsmann (38), kwa sasa analiongoza benchi la ufundi la timu ya taifa ya Ujerumani, hivyo Liverpool italazimika kusubiri hadi mkataba wake utakapokwisha baada ya Kombe la Dunia hapo mwakani.
Published:


