LONDON, Uingereza
KLABU za Ulaya zinaendelea kumwaga mishahara minono kwa nyota wao, huku zile za Ligi Kuu ya England zikitajwa kuongoza.
Katika makala haya, hawa ni wachezaji wa kandanda wanaopokea fedha nyingi zaidi kila wiki katika klabu zao.
Erling Haaland (Man City)
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, mpachikaji mabao huyo wa kimataifa wa Norway ndiye mchezaji anayelipwa zaidi si tu England, bali Ulaya kwa ujumla.
Haaland anavuna euro 608,922 kwa wiki katika klabu yake ya Manchester City. Ni sawa na kitita cha euro milioni 31 kwa mwaka. Mkataba wake utakwisha mwaka 2034.
Kylian Mbappe (Real Madrid)
Licha ya Madrid kukosa mataji yote msimu uliopita, Mbappe alifunga mabao 44. Mfaransa huyo alitwaa tuzo ya mfungaji bora wa Ulaya.
Ni kutokana na uwezo wake huo uwanjani, nyota huyo wa zamani wa PSG anavuna kiasi cha euro 600,962 kwa wiki pale Santiago Bernabeu.
Harry Kane (Bayern Munich)
Tangu alipofungua msimu huu wa 2025-26 kwa ‘hat-trick’ katika mchezo dhidi ya RB Leipzig, Kane ameendelea makali yake ya kuzifumania nyavu.
Mchango wake wa mabao kikosini unawafanya mabosi wa Bayern wasione tabu kumlipa mshahara wa euro 480,769 kwa wiki.
Mohamed Salah (Liverpool)
Nyota huyo wa kimataifa wa Misri alimaliza mkataba wake msimu uliopita na kupongeza mwingine Aprili, mwaka huu. Ni mkataba utakaokwisha mwaka 2027.
Kwa sasa, Salah ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi barani Ulaya, akiwa anapokea euro 463,940 kwa wiki.
David Alaba (Real Madrid)
Nafasi ya tano katika orodha ya wachezaji wanaolipwa mishahara minono zaidi barani Ulaya. Alaba anapokea euro 432,692 kwa wiki.
Nyota huyo wa kimataifa wa Austria alisajiliwa na Madrid mwaka 2021 akiwa mchezaji huru aliyemaliza mkataba wake Bayern Munich.
Dusan Vlahovic (Juventus)
Akitokea Fiorentina, Juventus walimsajili wakiwa na matumaini makubwa ya kumuona straika huyo akiendeleza ubora wake wa kupachika mabao.
Licha ya kushindwa kuwika tangu aliposajiliwa, bado Vlahovic analipwa euro 427,308 kwa wiki katika klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).
Casemiro (Man United)
Kwa sasa, Brazil huyo amerejesha makali yake ya kutawala eneo la kiungo. Ni baada ya miezi mingi ya kuonekana ameshuka kiwango.
Mabosi wa Manchester United wanamlipa nyota huyo mshahara wa euro 405,948 kwa wiki. Ni kama anavyolipwa Virgil van Dijk katika klabu ya Liverpool.
Manuel Neuer (Bayern Munich)
Kwa miaka mingi ya hivi karibuni, Neuer amekuwa kipa namba moja wa Bayern Munich na timu yake ya taifa ya Ujerumani. Bayern wanamlipa euro 403,846 kwa wiki.
Neuer ataendelea kuvuna kiasi hicho cha fedha hadi atakapomaliza mkataba wa mwaka mmoja aliosaini hivi karibuni.
Robert Lewandowski (Barcelona)
Staa huyo wa Barcelona analipwa euro 400,577, kama ilivyo kwa Jude Bellingham na Vinicius Jr (Real Madrid), Jan Oblak (Atletico Madrid) na Joshua Kimmich (Bayern Munich).
Kwa mujibu wa ripoti zilizopo, mshambuliaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund na Bayern Munich ataondoka Camp Nou mwishoni mwa msimu huu wa 2025-26.
Published:


