19.5 C
New York

Makocha hawa kiboko kwa kadi nyekundu

Published:

LONDON, Uingereza
WAKATI mwingine, makocha wamejikuta wakizidiwa na presha ya kile kinachoendelea uwanjani na mwishowe kuadhibiwa kwa kadi nyekundu.
Ni kama ilivyotokea kwa makocha hawa, ambao rekodi zinawatambua kwa idadi kubwa ya kadi nyekundu walizolimwa.
Jose Mourinho (9)
Katika msimu wake wa kwanza Chelsea, kocha huyo wa kimataifa wa Ureno alilimwa kadi nyekundu mbili kwa nyakati tofauti, akitozwa faini ya jumla ya Pauni 8000.
Alipokwenda kuinoa AS Roma ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A), Mourinho ‘Special One’ alikumbana na kadi nyekundu tano.
Pia, alipata kadi zingine mbili katika kibarua chake cha mwisho akiwa mkuu wa benchi la ufundi la vigogo wa soka la Uturuki, Fenerbahce.
Diego Simeone (7)
Kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina amezizoa kadi nyekundu zote hizo akiwa mkuu wa benchi la ufundi la Atletico Madrid.
Simeone amekuwa kwenye benchi la timu hiyo tangu mwaka 2011. Ndiye kocha aliyedumu na timu moja kwa muda mrefu zaidi katika Ligi Kuu zote tano za Ulaya.
Kama itakumbukwa, kadi yake ya mwisho alilimwa katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2014.
Xavi Hernandez (3)
Katika maisha yake ya ukocha, kiungo huyo wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania alilimwa kadi nyekundu tatu.
Ifahamike kuwa Xavi alipata kadi zote hizo katika miaka yake miwili na nusu akiwa kwenye benchi la ufundi la Barcelona.
Andre Villas Boas (3)
Kocha huyo wa kimataifa wa Ureno hakuwahi kulimwa kadi nyekundu kwa kipindi chote alichofanya kazi England akiwa na Chelsea na Tottenham.
Kama haijasahaulika, kadi yake ya mwisho alikutana nayo akiwa kocha wa vigogo wa Ligue 1, Marseille. Ni katika mchezo wa sare ya mabao 2-2 na Amiens mwaka 2020.
Arsene Wenger (3)
Moja ya kadi nyekundu maarufu za kocha huyo akiwa Arsenal ni aliyoipata katika mchezo dhidi ya Manchester United pale Old Trafford kwa kitendo chake cha kuipiga teke chupa ya maji.
Katika siku za mwisho wa maisha yake ya ukocha, alipewa kadi nyekundu mwaka 2017 kwa utovu wa nidhamu aliouonesha baada ya Burnley kupewa penalti katika mchezo ambao Arsenal ilishinda mabao 2-1.

Related articles

Recent articles