BERN, Uswis
MWAKA 1993, Uswis ilikuwa moja ya mataifa makubwa katika ulimwengu wa soka, ambapo ilishika nafasi ya tatu kwenye viwango vya ubora. Kwa sasa, iko nafasi ya 17.
Katika fainali zilizopita, iliendeleza majanga yake ya kuishia hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Dunia. Ilitolewa kwa kichapo cha aibu cha mabao 6-1.
Kwa misimu mitatu ya hivi karibuni, Uswis ambayo hii ni mara yao ya 13 kushiriki, haijaweza kuingia robo fainali ya mashindano hayo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Ikimaanisha, ‘Rossocrociati’ watakwenda katika fainali zijazo wakiwa na mtihani wa kuingia kwa mara ya kwanza robo fainali tangu walipogusa hatua hiyo mwaka 1954.
Kikosi chao kina mastaa kadhaa wanaokipiga barani Ulaya, ikitosha kuwataja Granit Xhaka (Sunderland), Breel Embolo (Rennes) na Manuel Akanji (Inter Milan).
Pia, mshambuliaji mzaliwa wa Cameroon, Breel Embolo, ndiye aliyeibeba zaidi Uswis katika mechi za kufuzu, ambapo alifunga mabao manne.
Kocha wao ni Murat Yakin, ambaye ana miaka minne kwenye benchi la ufundi tangu alipoajiriwa Agosti, 2021.
Yakin, ambaye alicheza mechi 49 akiwa mchezaji wa Uswis, ni kaka wa staa wa zamani wa timu hiyo, Hakan, aliyefunga mabao 20 katika mechi 87.
Published:


