PRETORIA, Afrika Kusini
KWA sasa, Afrika Kusini iko nafasi ya 61 katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Iliwahi kuwa ya 16 mwaka 1996.
‘Bafana Bafana’, licha ya utajiri wa vipaji vya kandanda, huku klabu zake zikiwa na mafanikio makubwa Afrika, ni mabingwa mara moja pekee wa fainali za Mataifa Afrika (AFCON).
Chini ya Hugo Broos, ambaye amekuwa kwenye benchi la ufundi tangu Mei, 2021. Raia huyo wa Ubelgiji aliiongoza kushika nafasi ya tatu msimu uliopita wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023).
Historia inakumbusha kuwa Bross alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Ubelgiji iliyoshika nafasi ya nne katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1986 zilizofanyika Mexico.
Akiwa ameshasema atastaafu baada ya Kombe la Dunia mwakani, ana kikosi chenye mastaa Teboho Mokoena na Aubrey Modiba (Mamelodi Sundowns) na Evidence Makgopa (Orlando Pirates).
Pia, wapo Jayden Adams, Oswin Appolis, Lyle Foster na Thapelo Morena, ambao wote walifunga katika mechi za kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia hapo mwakani.
Afrika Kusini inashiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu ilipokuwa mwenyeji mwaka 2010. Haijawahi kuvuka hatua ya makundi mara zote tatu ilizocheza michuano hiyo.
Published:


