Na mwandishi wetu, Gazetini
BAADA ya kuandika historia ya kufika makundi, sasa Singida Black Stars inawinda rekodi nyingine ya kushinda mechi kwenye hatua hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ni Novemba 23, mwaka huu, ambapo Singida BS itakuwa ugenini nchini Algeria kumenyana na CR Belouizdad, mchezo wa kwanza wa Kundi C, ambalo pia lina Stellenbosch FC (Afrika Kusini) na AS Otoho (Congo Brazzaville).
Je, ni nani hao CR Belouizdad? Kwa ufupi, ni mabingwa mara 10 wa taji la Ligi Kuu ya Algeria, ingawa mara ya mwisho kutwaa ubingwa ilikuwa msimu wa 2022-23.
Kuingia kwao hatua ya makundi kulitokana na ushindi wa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya Haifa ya Guinea. Mechi ya kwanza ilichezwa Guinea na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Msimu huu, wanashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakiwa wamecheza mechi tisa (wameshinda tatu, sare tatu na kufungwa moja).
Kama ilivyo kwa Singida yenye Miguel Gamondi, CR Belouizdad nao wananolewa na kocha aliyewahi kuliongoza benchi la ufundi la Yanga, Ramovic Sead.
Wakati huo huo, hata Gamondi amewahi kuinoa CR Belouizdad, ambapo alikaa kwenye benchi la ufundi kwa mwaka mmoja (Julai 4, 2010 – Juni 30, 2011).
Katika mechi tisa za Ligi walizocheza msimu huu, wamefunga mabao 10 pekee lakini safu yao ya ulinzi imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.
Ifahamike kuwa beki Youcef Laouafi ndiye mchezaji aliyeifungia mabao mengi zaidi msimu huu wa Ligi, akiwa ameingia kambani mara tatu.
Kwa mechi za kimataifa inapokuwa nyumbani, CR Belouizdad hutumia Uwanja wa Nelson Mandela unaoingiza mashabiki 40,784. Ni mali ya Shirikisho la Soka la Algeria.
Published:


