Na Hassan Mwasha, Gazetini
YANGA wako Kundi B msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo wamepangwa na Al Ahly ya Misri, AS FAR (Morocco) na JS Kabylie (Algeria). Yanga, baada ya kuishia hatua ya makundi msimu uliopita, safari hii malengo ni kupiga hatua kubwa zaidi, ikiwamo kuvuka robo fainali waliyofika mwaka 2023.
Safari hii, ili kufika hatua ya makundi, wawakilishi hao wa Tanzania walizitoa Wiliete SC ya Angola (2-1) na Silver Strikers ya Malawi (2-1). Kuelekea mchezo wa kwanza wa makundi dhidi ya AS FAR utakaochezwa Novemba 21, mwaka huu, makala haya yanakuibulia mambo 12 kuhusu wapinzani hao wa Yanga.
Mosi, AS FAR ilianzishwa mwaka 1958, miaka mitatu tu baada ya Moroccco kupata uhuru wake kutoka kwa wakoloni (Ufaransa). Pia, katika ushiriki wao mara 13, wametwaa mara moja taji la Ligi ya Mabingwa, ingawa wamecheza fainali mara tatu. Msimu uliopita, waliishia robo fainali.
Lakini, licha ya kwamba ni miongoni mwa klabu kubwa katika soka la Morocco, AS FAR haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu tangu ilipofanya hivyo msimu wa 2022-23. Hata hivyo, isisahaulike kuwa wakati Yanga wakiifunga KMC mabao 4-1, AS FAR wametoka kulamizimishwa suluhu (0-0) dhidi ya MAS Fes katika mchezo wa Ligi Kuu ya Morocco uliochezwa Jumapili ya Novemba 9, mwaka huu.
Mbali ya hilo, msimu huu AS FAR inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Morocco ikiwa na pointi 18, ikizidiwa mbili na Wydad Casablanca. Ikumbukwe pia, katika mechi nane ilizoshuka dimbani msimu huu wa Ligi, FAR Rabat haijafungwa, na badala yake imeshinda tano na kutoa sare tatu.
Vilevile, ikiwa imefunga mabao 14 katika mechi nane za Ligi, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu, ikithibitisha ubora wa safu yake ya ulinzi. Usichokijua, kinara wa mabao wa kikosi hicho ni kiungo Mohamed Hrimat, ambaye ana mabao matano msimu huu wa Ligi Kuu. Hrimat ni miongoni mwa wachezaji ghali zaidi Afrika kwa sasa.
Kwa upande mwingine, AS FAR imefika hatua hii ya makundi kwa kuziondoa Real Banjul ya Gambia (4-1) na na Horoya ya Guinea (4-1). Aidha, timu hiyo haijafungwa ugenini msimu huu wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa. Imeshinda mechi tatu na kutoa sare mbili.
Wakati huo huo, kocha ni raia wa Ureno, Alexandre Santos, ambaye ana uzoefu mkubwa katika soka la Afrika kwani amewahi kuzinoa Atletico de Luanda (Angola) na CS Sfaxien (Tunisia). Mwisho, AS FAR ni waumini wa mfumo wa 4-2-3-1, ambao amekuja nao kocha huyo mwenye leseni ya UEFA Pro.


