7.8 C
New York

Barua ya wazi kwa ‘Goli la Mama’

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KWAKO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan. Nianze kwa kupongeza juhudi za Serikali yako katika kupigania maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini. Hongera!
Kwetu wapenzi wa soka, ni bahati na fursa iliyoje kuwa na kiongozi mwenye ndoto za kuona mchezo huo unapiga hatua kubwa na kuitangaza nchi kwenye medani ya kimataifa.

Kuthibitisha ulivyo na nia thabiti ya kuliona soka letu linapiga hatua, nitatolea mfano namna ambavyo Dkt. Samia umekuwa bega kwa bega na timu za Tanzania zinazoshiriki michuano ya kimataifa kupitia ‘Goli la Mama’.

Kupitia kampeni hiyo, Serikali yako imekuwa ikizawadia kiasi cha Shilingi milioni tano kwa kila bao linalofungwa na timu zetu zinazoiwakilisha nchi katika mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Klabu kongwe za Simba na Yanga zimekuwa wanufaikaji wakubwa wa fedha hizo kupitia ushiriki wao Ligi ya Mabingwa, kama ilivyo kwa Azam FC na Singida Black Stars msimu huu wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Niseme tu, ni kutokana na sapoti kubwa hiyo ya ‘Goli la Mama’, Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia, imeingiza timu nne (Simba, Yanga, Azam na Singida BS) kwa mkupuo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, binafsi kuna jambo ningependa kushauri ili kampeni hiyo ya ‘Goli la Mama’ iweze kuleta tija zaidi katika ustawi wa mchezo wa soka hapa nchini. Nianze hivi; maendeleo ya soka, kama ilivyo kwa michezo mwingine duniani kote, hutokana na msingi imara uliojengwa kuanzia ngazi za chini.

Leo hii, maendeleo ya soka letu hayawezi kupimwa kwa klabu za Simba na Yanga kufika robo fainali, fainali au hata kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa. Ni hadi pale tutakapokuwa na msingi imara katika ujenzi wa maendeleo ya mchezo huo. Msingi upi? Ni uwekezaji mkubwa katika soka la vijana.

Namaanisha, tunaweza kuwa na uhakika wa kesho ya soka letu endapo ‘Goli la Mama’ ingegeuka sasa na kujikita katika uzalishaji wa utititi wa vituo vya kuibua na kukuza vipaji katika ngazi za kata na wilaya.
Kupitia vituo hivyo, tutakuwa na kesho iliyo bora kwa vijana wa U-17 na U-20 na matumaini ya kuiona Tanzania ikifanya vizuri katika fainali za Mataifa Afrika (AFCON), fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), na hata Kombe la Dunia.

Ndicho walichokifanya wenzetu wa Morocco, ambao uwekezaji wao mkubwa ulielekezwa katika soka la vijana na sasa timu ya taifa, pamoja na klabu zao, ni tishio katika mashindano makubwa ya ndani na nje ya Afrika.
Kwa upande mwingine, kuwekeza zaidi katika ujenzi wa vituo hivyo utaimarisha uchumi wa klabu zetu kwa kuepuka mzigo mkubwa wa kusajili wachezaji wa kigeni inaowategemea kwa sasa.

Tuitazame tena Morocco. Kama zilivyo Misri na Algeria, klabu zao zinazofanya vizuri Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika zinategemea kwa kiasi kikubwa wachezaji wa ndani, waliopikwa na vituo vya kuibua na kukuza vipaji.

Nirudi kwako Dk. Samia. Nisisitize pongezi zangu kwa ‘Goli la Mama’, wakati huo pia nikiomba sasa kampeni hiyo isiendelee kubeba taswira ya motisha, na badala yake itumike katika mikakati ya soka la vijana.
Walau kuwa na vituo viwili vikubwa vya soka la vijana katika kila wilaya kutatupa matumaini ya kuiona kesho bora ya soka letu kupitia U-17, U-20 na Taifa Stars, kuliko Simba au Yanga kuwa bingwa msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Asante.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img