7.8 C
New York

Kufanya vizuri AFCON, kupanga ni kuchagua!

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
KWA miaka sita ya hivi karibuni, timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imefuzu mara tatu fainali za Mataifa Afrika (AFCON). Ilifanya hivyo mwaka 2019, 2021 na sasa itashiriki michuano ya mwaka huu huko Morocco.
Ilipofuzu mwaka 2019, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kutia mguu kwenye mashindano hayo tangu ilipokata tiketi mwaka 1980.
Hivyo, ni mafanikio makubwa kwa soka la Tanzania kuona Stars ikishiriki mara tatu fainali hizo kwa kipindi kifupi tu cha miaka sita (tangu 2019) ya hivi karibuni.
Lakini, changamoto kubwa iliyopo ni kukosekana kwa mipango itakayoliwezesha soka la Tanzania kunufaika na fursa hiyo ya kushiriki fainali hizo.
Isivyo bahati, kila Stars inapokata tiketi, matumaini yamekuwa ni kuiona ikifanya vizuri kwenye michuano hiyo. Ndoto imekuwa ni kuinoa Stars ikifanya ‘maajabu’.
Hata hivyo, licha ya matumaini makubwa, Stars haijawahi kuvuka hatua ya makundi kwenye fainali hizo. Imeishia makundi mara zote mbili za hivi karibuni.
Nini kifanyike, hasa kuelekea fainali zijazo za AFCON zitakazoanza Desemba, mwaka huu, na kumalizika Januari, mwakani? Tujadili.
Ukweli ulio wazi ni kwamba bado hakuna mikakati ya kuitumia michuano hiyo kulinufaisha soka la Tanzania kwa ujumla. Na badala yake, imekuwa ikishiriki kwa mazoea.
Mikakati ninayoizungumzia ni kuandaa timu itakayokwenda kumudu ushindani na si kusindikiza mataifa mengine kwenye mashindano. Je, hilo litawezekana kwa namna gani?
Ni kwa kuandaa timu ya muda mrefu, badala ya kutegemea muujiza kama ilivyo sasa. Lazima tuachane na ndoto za kufanya maajbu. Iwepo mikakati ya kuandaa timu walau kwa miaka miwili hadi mitatu.
Mathalan, wakati wa fainali za AFCON mwaka 2019, kikosi cha Stars kilipaswa kuundwa na walau asilimia 55 ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 23.
Kwamba wakati mataifa mengine yakipiga hesabu za ubingwa, Tanzania ilipaswa kutumia mashindano hayo kuandaa timu ya ushindani.
Kinyume chake, Tanzania ilikwenda kwenye mashindano ikiwa na matumaini ya kufanya maajabu, ikijiweka ‘levo’ moja na Misri, Ivory Coast na mataifa mengine yaliyopiga hatua kubwa kwenye soka.
Matokeo yake, si tu iliishia makundi, bali pia ilishindwa kutumia fursa hiyo kuandaa vijana, ambao wangeweza kuwa wameiva wakati wa fainali za msimu uliofuata (AFCON 2021). Stars ikaishia tena hatua ya makundi.
Ikiwa ni miezi takribani miwili tu kuelekea AFCON ya mwaka huu, mwendo ni ule ule. Hakuna ‘project’ ya vijana iliyoandaliwa kwa muda mrefu lakini matumaini ni kuinoa Stars ikifanya maajabu.
Endapo tungethubutu kuwatumia vijana wa U-23 katika fainali za AFCON mwaka 2021, huenda wangeshaiva na kutumika kwenye michuano ya CHAN iliyomalizika wiki chache zilizopita.
Matokeo yake, Tanzania ilifeli kuvuka makundi kwenye fainali za AFCON 2021 na pia ilivurunda katika michuano ya CHAN, licha ya kwamba ilikuwa mwenyeji wa michuano hiyo ikishirikiana na majirani zake wa Afrika Mashabiki, Kenya na Uganda.
Hatujachelewa. Tuanze sasa. Benchi la ufundi liache utamaduni wa kuita kikosi kilichojaza mastaa wenye uzoefu mkubwa, kana kwamba wana uwezo wa kutwaa ubingwa wa AFCON.
Na badala yake, fainali hizo ziwape nafasi kubwa wachezaji wenye umri mdogo, ambao wataisidia nchi hapo baadaye. Malengo yawe ni AFCON 2027 au mashindano mengine ya hapo baadaye.
Kinyume cha hapo, Stars haitafanya maajabu AFCON 2025 na pia tutakosa fursa ya kutumia michuano hiyo kutengeneza timu kwa ajili ya msimu ujao. Kupanga ni kuchagua!

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img