Na Hassan Mwasha, Gazetini
HIVI karibuni, klabu kongwe zaidi za soka nchini, Simba na Yanga, zilitangaza makocha wapya. Simba ilimuajiri, Dimitar Pantev, wakati Yanga walimpa ajira Pedro Goncalves.
Makocha wote wawili si tu ni mara yao ya kwanza kufanya kazi nchini, bali pia ni raia wa kigeni. Pantev anatokea Bulgaria, wakati Pedro Gonclaves ni raia wa Ureno.
Haishangazi tena. Ni mwendelezo wa klabu za Simba na Yanga kuwaamini wageni na kuwafungia milango ya ajira makocha wazawa.
Miaka michache iliyopita, Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’ walijaribu kumaliza utamaduni huo wa kuwapuuza makocha wa hapa nyumbani.
Itakumbukwa, Simba walimpa benchi la ufundi kocha mzawa, Juma Mgunda, ambaye alijiunga nao baada ya kazi nzuri aliyoifanya akiwa na kikosi cha Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’.
Hata hivyo, licha ya timu hiyo kuwa na matokeo mazuri kwenye mechi zake za Ligi ya ndani na zile za kimataifa, Mgunda alipokonywa kibarua hicho na kukabidhiwa kocha wa kigeni kutoka Brazil, Robertinho.
Mabingwa wa kihistoria Ligi Kuu Bara, Yanga, kwa miaka takribani 20 sasa, hawajathubutu kumuamini kocha mzawa.
Hata hivyo, utamaduni wa kutokuwaamini wazawa umeenda mbali zaidi kwa Wanajangwani hao, ambapo wamekuwa wakiajiri kocha wa kigeni hata kwenye nafasi ya msaidizi.
Wiki chache zilizopita, walimtangaza kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Malawi, Mabedi, kuwa kocha msaidizi kwenye benchi lao la ufundi.
Ni nafasi ambayo wangeweza kumpa mmoja kati ya makocha wazawa wengi waliopo hapa nchini.
Kwamba walau Simba, ambayo licha ya kutokuwaamini wazawa kwenye nafasi ya kocha mkuu, walau imeendelea kumpa nafasi ya usaidizi kiungo wake wa zamani, Suleiman Matola.
Kwanini makocha wa kigeni? Licha ya makocha wazawa kubezwa kuwa hawana vigezo vya kitaaluma, hoja hiyo inakosa nguvu kwa kuwatolea mfano Mgunda na kocha wa sasa wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Makocha hao wana elimu ya juu ya ufundishaji wa soka, kama ilivyo kwa wageni wanaokuja nchini, na wanakidhi vigezo vyote vya kuyaongoza mabenchi ya ufundi ya Simba, Yanga na klabu yoyote barani Afrika.
Ni kutokana na uwezo wao mkubwa, wameiwezesha Taifa Stars kukata tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) na Watanzania wataishuhudia timu yao ikishiriki michuano hiyo ya Desemba nchini Morocco.
Kwamba tatizo si vigezo vya kitaaluma, bali ni kasumba tu ya viongozi wa Simba na Yanga, wakiamini kuwa klabu inakuwa imepiga hatua kubwa inapoajiri kocha wa kigeni.
Mbaya zaidi, wamefanikiwa kuwaambukiza hata mashabiki na wanachama wao na sasa kuajiri kocha mzawa kunatafsiriwa kuwa ni hali mbaya ya kiuchumi kwa klabu.
Pia, hata wanapoajiri makocha wazawa, bado hawawapi hadhi sawa na ile ya wageni, ikiwa ni pamoja na kulipwa mishahara midogo na kuingiliwa katika maamuzi.
Je, ni makocha wa kigeni wangapi waliokuja hapa nchini na kuzipa mafanikio makubwa klabu za Simba na Yanga katika michuano ya kimataifa? Ni wachache, ukilinganisha na orodha ndefu ya wageni walioajiriwa katika miaka ya hivi karibuni.
Published:


