5.9 C
New York

Megawati 90 kuongeza uchimbaji madini Chunya – “umeme safi, uwekezaji bora”

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Alhaji Batenga, amefafanua mikakati kabambe ya kuimarisha shughuli za uchimbaji madini wilayani humo, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Umeme (Substation) chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 90, hatua inayolenga kupunguza changamoto za upatikanaji wa nishati kwa shughuli za madini na sekta nyingine.

Akizungumza katika mahojiano maalum na timu ya Madini Diary, Batenga alisema kituo hicho kitajengwa katika eneo la Makongorosi-Chunya na kitahudumia wilaya nzima pamoja na Mkoa wa Songwe. Alitaja mifano ya miradi ya madini inayofaidika na mradi huo, ikiwemo Mgodi mpya wa Shanta – New Luika, Mtambo wa uchenjuaji wa Anglo De Beers mpakani mwa Chunya na Songwe, na mgodi wa Porcupine North ulioanza baada ya upanuzi.

“Kwa sasa wilaya inatumia megawati 9 pekee, huku mahitaji halisi yakiwa si chini ya megawati 90. Kupitia kituo hiki, tutaanza kuzalisha megawati 45, lengo likiwa kufanikisha uchimbaji wa kisasa kwa gharama nafuu na kuhamasisha uwekezaji zaidi. Wachimbaji wanahitaji sana umeme, na nitalisimamia hili kikamilifu,” amesema Batenga.

Aliwapongeza wachimbaji wadogo na kutoa wito kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuipa kipaumbele kusambaza umeme katika maeneo yenye shughuli za madini ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija. Aliongeza kuwa, upatikanaji wa nishati safi utasaidia kuvutia uwekezaji zaidi kutokana na utajiri wa rasilimali madini wilayani humo, na kutaja ukuaji wa kampuni ya Anglo De Beers katika eneo la Chunya na Songwe.

Aidha, Batenga aliwapongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele sekta ya madini, hususan wachimbaji wadogo. Amesema wilaya hiyo imepata zaidi ya leseni 1,500 kwa wachimbaji wadogo, na aliomba kuendelea kutoa leseni zisizoendelezwa ili wachimbaji wenye nia waendelee kuchimba kwa uhakika.

Batenga pia aliwashauri wachimbaji kufanya tafiti za maeneo mapya ya madini kwa kutumia mitambo ya gharama nafuu, na kupongeza uanzishaji wa mitambo ya uchorongaji miamba.

Alibainisha kuwa wilaya ya Chunya ina tarafa mbili za kipekee, Kiwanja maalumu kwa madini na Kipambawe kwa kilimo cha tumbaku, na aliongeza kuwa wilaya inachangia asilimia 60 ya mapato ya maendeleo kwenye mfuko mkuu wa Serikali, ikitarajiwa kufikia asilimia 80 ndani ya miaka mitano ijayo kutokana na mapato ya madini na tumbaku.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img