Na mwandishi wetu, Gazetini
MATUMAINI ya mashabiki wa soka nchini kuiona timu yao ya Taifa, Taifa Stars, ikifuzu fainali zijazo za Kombe la Dunia yameota mbawa baada ya kufungwa bao 1-0 na Zambia ‘Chipolopolo’.
Stars ilipoteza mchezo huo wa jana ikiwa nyumbani katika Uwanja wa New Aman Complex, Zanzibar, hivyo kufikisha pointi 10. Matokeo hayo yameifanya Stars kushika nafasi ya tatu katika Kundi linaloongozwa na Morocco, ambayo imeshafuzu.
Niger, ambayo ilipata ushindi dhidi ya Congo Brazaville katika mchezo mwingine wa jana, inashika nafasi ya pili na walau ina matumaini ya kucheza ‘play off’ baada ya kufikisha pointi 12.
Kwa upande wake, Stars chini ya kocha mzawa, Hamed Suleiman ‘Morocco’, haina tena nafasi ya kwenda Kombe la Dunia na sasa inajipanga kwa ajili ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Desemba, mwaka huu.
Ukiwa ni mfuatiliaji mzuri wa safari ya Stars katika mbio za kuwania tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia, utagundua kuwa bado Watanzania wanahitaji subra ya muda mrefu kuiona timu yao ikifuzu michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Changamoto kubwa kwa Stars ni namna ya kutumia nguvu ya mashabiki inapocheza katika uwanja wake wa nyumbani. Hilo lilithibitika katika michezo miwili, ambayo matokeo yake ndiyo yaliyotibua safari ya Stars kukata tiketi.
Kama itakumbukwa, Stars ilikuwa na nafasi nzuri ya kujisafisha njia endapo ingepata ushindi katika mchezo wake wa nyumbani dhidi ya Niger. Katika mazingira ya kushangaza, ilikubali kipigo cha bao 1-0.
Endapo Stas ingepata ushindi huo, ingekutana na Zambia ikiwa tayari imefikisha pointi 13. Kwamba hata kama ingefungwa na Zambia, bado ingeshika nafasi ya pili baada ya Niger kuifunga Congo Brazaville.
Dhidi ya Chipolopo katika mchezo wa usiku wa jana, bado kete ilikuwa upande wa Stars, hasa baada ya ushindi wake wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika ardhi ya Zambia.
Ikiwa mbele ya mashabiki wake Visiwani Zanzibar, ilihitaji ushindi tu ili kufikisha pointi 13, ambazo Niger isingezifikia hata baada ya kupata ushindi wa nyumbani mbele ya Congo.
Hesabu ni rahisi tu. Uzoefu wa soka la Afrika unaonesha kuwa timu zinahitaji zaidi matokeo ya mechi za nyumbani ili kufanya vizuri katika hatua za aina hii.
Stars haijaonekana kujifunza katika hilo. Kama ilivyoonekana katika mechi dhidi ya Niger na Zambia, bado Stars imeonekana kuwa ni nyepesi kupoteza ikiwa mbele ya mashabiki wake.
Tunaweza kujikumbusha kilichotokea katika fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN)? Stars ikiwa mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, bado haikunufaika na nguvu ya mashabiki wake.
Hivyo, katika mazingira ya kutegemea ‘bahati’ ya ushindi wa michezo ya ugenini, huku ikishindwa kunufaika na uwanja wa nyumbani, ni ngumu kwa kiasi fulani kuamini kuwa Stars inaweza kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
Published:


