13.1 C
New York

Vijana Afrika na ndoto za maisha bora Ulaya

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

TAKRIBANI asilimia 60 ya vijana wa Afrika wanaamini watapata maisha bora endapo wataondoka na kwenda ‘kupambana’ nje ya Bara hili.

Wengi wao wanasukumwa na maisha duni wanayoishi katika nchi zao, ikichagizwa na uhaba wa ajira, uhaba wa huduma za kijamii, rushwa, na mengineyo yenye kuwakatisha tamaa.

“Rushwa imeibua sintofahamu kubwa juu ya hatima ya vijana,” anasema Someleze Sigudu, raia wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 28, akiongeza kuwa vitendo vya rushwa, hasa Serikalini, vimewakatisha tamaa vijana wengi nchini humo.

Kupitia ripoti yake ya mwaka jana, Taasisi ya African Youth Survey ilionesha kuwa vijana zaidi ya 5,600 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24 barani Afrika walipaza sauti kulaani vitendo vya rushwa katika mataifa yao.

Utafiti huo uliangazia maoni ya vijana katika mataifa ya Botswana, Cameroon, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ivory Coast, Ethiopia, Gabon, Ghana, Kenya, Malawi, Namibia, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, Tanzania na Zambia.

Sigudu, kwa upande wake, anaamini Serikali yake ya Afrika Kusini haijafanya vya kutosha katika kukabiliana na rushwa. “Bado viongozi wanaokutwa na hatia hawaadhibiwi,” anasema.

Anasisitiza kuwa vitendo vya rushwa vimekuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa matatizo mengine kwa vijana, ikiwamo ukosefu wa ajira.

Ikumbukwe, Afrika Kusini ni moja ya mataifa yenye kiwango kikubwa cha uhaba wa ajira, ambapo asilimia zaidi ya 41 ya wahitimu wa elimu ya juu walishaacha kutafuta nafasi za kazi baada ya miaka mingi ya kusota mitaani.

Lucy Ntshangase, kijana mwenye umri wa miaka 31, ni miongoni mwao na sasa anaweka wazi kuwa mpango wake ni kutimkia Ulaya akiamini atakwenda kutimiza ndoto zake. “Huu ni mwaka wa tatu sasa nahangaika kutafuta kazi,” anasema.

Naye mchambuzi wa siasa nchini Afrika Kusini, Sandile Swana, anawatupia lawama wanasiasa wa Chama tawala, African National Congress (ANC), akisema kundi hilo ndiyo chanzo kikubwa cha tatizo la rushwa.
“Watu wachache wamejimilikisha Serikali, wao ndiyo wanaopanga kila kitu. Ni ngumu hata kuwavutia wawekezaji wa nje kuja Afrika Kusini,” anasema Swana katika mahojiano yake na DW.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img