LONDON, England
NI mapema mno lakini tayari baadhi ya klabu zinaonesha dalili ya kushuka daraja msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL). Ikumbukwe, timu zote 20 zimeshashuka dimbani mara tatu tangu msimu ulipoanza wiki chache zilizopita.
BURNLEY
Chini ya kocha Scott Parker, Burnley inaonesha dalili zote za kurejea Ligi Daraja la Kwanza (Championship).
Burnley inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa EPL baada ya kushuka dimbani mara tatu. Walifungua pazia kwa kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Tottenham, kisha ‘wakafufuka’ kwa ushindi wa 2-0 mbele ya Sunderland.
Baada ya hapo, walipoteza kwa kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Manchester United. Kwamba Parker na vijana wake wamekusanya pointi tatu pekee kati ya tisa walizopaswa kuwa nazo kufikia hatua hii.
WOLVES
Wako mkiani kabisa mwa msimamo na ni matokeo ya kupoteza mechi zote tatu walizocheza. Mechi yao ya kwanza ni ile waliyopokea kipigo kizito cha mabao 4-0 kutoka kwa Manchester City ya Pep Guardiola. Ni kutokana na mwenendo wao, Wolves wako kwenye nafasi nzuri ya kuiaga EPL mwishoni mwa msimu huu.
SUNDERLAND
Wamerejea EPL na kuanza vizuri msimu huu, ingawa bado wana kazi ya kufanya ili kujinasua katika nafasi ya kushuka daraja.
Sunderland walishinda mechi yao ya kwanza, wakiifunga West Ham mabao 3-0 lakini wakafungwa 2-0 na Burnley. Hata hivyo, walirejea kwenye kasi yao ya ushindi walipoifunga Brentford bao 1-0 katika mchezo waliokuwa nyumbani.
LEEDS UNITED
Baada ya kuuanza msimu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Everton, Leeds walipoteza mechi iliyofuata.
Walifungwa mabao 5-0 na Washika Bunduki wa London, Arsenal, kabla ya kupata sare mbele ya Newcastle United. Leeds wako nafasi ya 12 kwenye msimamo wa EPL, hivyo ni wazi wanaweza kushuka daraja endapo hawatakaza buti.
BRENTFORD
Balaa lilianzia wakati wa usajili wa kiangazi, ambapo iliwapoteza watu muhimu, akiwamo kocha Thomas Frank aliyetimkia Tottenham. Pia, kikosi hicho kiliwapoteza wachezaji waliokuwa wakiibeba, wakiwamo Bryan Mbeumo, Yoane Wissa, Christian Norgaard na Mark Flekken.
Walifungua msimu kwa kufungwa na Nottingham Forest, kabla ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Aston Villa, kisha kufungwa na Sunderland.
WEST HAM UNITED
Ni wazi wakali hao wa Magharibi mwa Jiji la London wako hatarini. Waliuanza msimu kwa kufungwa mechi mbili, kabla ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nottingham Forest.
Huenda hali ya ‘Wagonga Nyundo’ ikawa mbaya zaidi endapo itafungwa na Tottenham katika mchezo ujao wa ‘derby’ ya London.
Published:


