9.8 C
New York

City v United … Guardiola kumfukuzisha kazi Amorim?

Published:

MANCHESTER, Uingereza
NI Jumapili ya wiki hii, ambapo nyasi za Uwanja wa Etihad zitabeba uzito wa dakika 90 za ‘derby’ ya jijini Manchester.
Manchester City watakaokuwa nyumbani dhidi ya wapinzani wao wakubwa, Manchester United, ukiwa ni mtangange wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Man City waliuanza vizuri msimu huu kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 katika mchezo wa ugenini dhidi ya Wolves. Mechi hiyo ilifuatiwa na vichapo viwili mfululizo kutoka kwa Tottenham (2-0) na Brighton (2-1).
Matokeo hayo ya mechi tatu yanaifanya Man City kushika nafasi ya 13 katika msimamo wa EPL.
Kwa upande wao, Man United inayoshikilia nafasi ya tisa, ilifungua pazia la msimu huu EPL kwa kichapo cha bao 1-0 ikiwa nyumbani (Old Trafford) dhidi ya Arsenal.
Baada ya mchezo, walipata sare mbele ya Fulham na kisha ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Burnley.
Ulinzi v Ushambuliaji
Kwa takwimu za mechi nne, ni rahisi kuona kuwa timu zote zina ubora kwenye ushambuliaji lakini bado safu za ulinzi ni tatizo.
Man City, licha ya kufunga mabao matano katika mechi tatu, safu ya ulinzi imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne. Hali iko hivyo pia kwa Man United. Katika mechi tatu, imefunga mabao manne na kuruhusu manne.
Hivyo, kwa wabashiri wa matokeo ya soka, ni rahisi kuamini kuwa mchezo huo utamalizika kwa kila timu kufunga na kuruhusu bao.
Mastaa hawa kukosekana
Man City inatarajiwa kuwakosa Rayan Cherki na Mateo Kovacic, ambao walifanyiwa upasuaji. Licha ya taarifa ya Savinho kurejea mazoezini, John Stones ameumia, hivyo kuungana na Rico Lewis, Abdukodir Khusanov na Rayan Ait-Nouri.
Man United, kwa upande wao, huenda ikacheza bila Matheus Cunha, Mason Mount na beki wa kati, Lisandro Martinez.
Rekodi
Man United ilizoa pointi nne katika ‘derby’ mbili za EPL msimu uliopita, ukiwamo ushindi wa mabao 2-1 ikiwa ugenini katika Uwanja wa Etihad.
Katika mechi tano za hivi karibuni, Guardiola ameifunga Man United mara moja pekee, akifungwa mbili na kuambulia sare mbili.
Amorim kutimuliwa?
Zipo taarifa kuwa kibarua cha kocha Ruben Amorim kinaweza kuota nyasi endapo atapoteza mechi mbili zijazo.
Wiki moja baada ya kumalizana na Man City, Amorim atakuwa na mtihani mwingine wa kujinasua mbele ya Chelsea pale Old Trafford.
Lakini, aliyewahi kuwa msaidizi wa kocha Alex Ferguson katika benchi la ufundi la Man United, Mick Brown, anasema:
“Sidhani kama atafukuzwa, hata kama atapoteza mechi zote mbili, ingawa maswali yatakuwa mengi juu ya uwezo wake wa kuisaidia timu.”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img