LONDON, Uingeereza
JOSE Mourinho, maarufu zaidi kwa jina la ‘Special One’, hana kazi kwa sasa baada ya klabu ya Fenerbahce kumfungashia virago hivi karibuni.
Mourinho alifutwa kazi akiwa amekalia benchi la ufundi kwa kipindi kisichozidi miezi 14 tu.
Uamuzi wa kumfuta kazi ulikuja baada ya mabosi wa Fenerbahce kukasirishwa na matokeo ya kufungwa bao 1-0 na Benfica katika mchezo wa ‘play-off’ ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pia, alishindwa kuipa timu hiyo taji la Ligi Kuu, akimaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita.
Hata hivyo, nje ya uwanja, tayari Mourinho raia wa Ureno alikuwa na uhusiano mbaya na mabosi wa klabu hiyo, akiwamo Rais wao, Ali Koc.
Chanzo cha ‘bifu’ ni Mourinho kukosoa mara kadhaa, tena kwenye vyombo vya habari, aina ya usajili unaofanywa na mabosi wake klabuni hapo.
Kwa mtazamo wake, usajili wa Fenerbahce hauoneshi kuwa ni klabu yenye ubavu wa kufanya vizuri, hasa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kama hiyo haitoshi, alikosoa namna klabu hiyo inavyolipa mishahara mikubwa kwa wachezaji anaoamini wana uwezo wa kawaida ndani ya uwanja.
Lakini, si tu kwa mabosi wake, pia Mourinho mwenye umri wa miaka 62 alikuwa mkosoaji mkubwa wa soka la Uturuki, hasa waamuzi wa Ligi Kuu, akisema hawana sifa za kupewa kazi hiyo.
Je, ni wapi anakoelekea kocha huyo wa zamani wa Porto, Chelsea, Real Madrid na Inter Milan baada ya kuachana na Fenerbahce?
Swali hilo linatokana na ukweli kwamba Mourinho ameshaweka wazi kuwa hana mpango wa kustaafu.
Ni kweli anakiri kukitamani kibarua cha kuinoa timu ya taifa ya Ureno lakini kwa sasa nafasi hiyo inashikwa na Roberto Martinez anayekiandaa kikosi kwa ajili ya fainali zijazo za Kombe la Dunia.
Hivyo basi, kutua West Ham United inaweza kuwa fursa iliyopo mbele yake zaidi kwa sasa. Kocha Graham Potter anahusishwa na mpango wa kufutwa kazi.
Mourinho ana uzoefu mkubwa wa kufanya kazi jijini London. Kwa nyakati tofauti, aliwahi kuzinoa Chelsea na Tottenham.
Pili, fursa nyingine kwake ni kwenda kuzifuata fedha za klabu tajiri huko Saudi Arabia.
Hiyo ni pamoja na kwenda kufanya kazi na Cristiano Ronaldo katika klabu ya Al-Nassr inayopigania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Endapo itatokea, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Mourinho kufanya kazi nje ya Ligi za barani Ulaya. Atakubali?
Wakati huo huo, pia kuna ajira inayomfaa katika klabu ya Leeds United. Klabu hiyo ina kocha wake wa muda mrefu, Daniel Farke, lakini fedha nyingi zilizotumika kwenye usajili zitashawishi kuhitaji mtu mwenye uzoefu zaidi ili kuipaisha klabu hiyo.
Aidha, kurudi Manchester United ni fursa nyingine kwa Mourinho. Atakumbukwa kuwa ni kocha aliyeiwezesha kumaliza msimu ikiwa nafasi ya pili, pia akiipa mataji mawili (Ligi ya Europa na Kombe la Ligi).
Kwa sasa, anayeinoa Man United ni Mreno mwenzake, Ruben Amorim, ambaye hata hivyo ni kama mambo hayaendi.
Published:


