13.1 C
New York

Afrika ‘jalala’ la wahamiaji haramu kutoka Marekani?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
UGANDA imeungana na Eswatini, Sudan Kusini na Rwanda kuingia mkataba wa kupokea wahamiaji haramu wasiotakiwa nchini Marekani.
Kuwaondosha wahamiaji haramu ni moja ya sera za Rais Donald Trump katika awamu yake ya pili madarakani, akiwa ameahidi kuisafisha Marekani.
Awali, wakati Rais Trump akiwania kiti cha urais katika Uchaguzi wa mwaka jana, kuwaleta wahamiaji barani Afrika haikuwa sehemu ya mipango ya utekelezaji wa sera hiyo.
Sudan Kusini na Eswatini zilitangulia kuingia makubaliano ya kupokea wahamiaji kutoka Marekani. “Julai (mwaka huu), kuna wahamiaji kadhaa walipelekwa Sudan Kusini na Eswatini. Ni wahamiaji wachache, wasiozidi 10,” anasema mchambuzi wa siasa, Alex Vines.
Kwa upande wa Uganda, hatua ya kupokea wahamiaji kutoka Marekani imeonekana kuacha maswali mengi, ikizingatiwa kuwa tayari ndilo Taifa lenye wakimbikizi wengi (zaidi ya milioni 1.7) barani Afrika.
Mzigo huo wa wakimbikizi unatokana na migogoro inayoendelea katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini.
Hata taarifa ya awali kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Henry Oryem Okello, ilieleza kuwa Taifa hilo la Afrika Mashariki halitakubali kubeba mzigo wa kupokea wahamiaji.
Kinyume chake, Uganda iliingia mkataba na Marekani, licha ya Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Vincent Bagiire, kuyaita kuwa ni ‘makubaliano ya muda mfupi tu’.
Lakini, kwa baadhi ya raia wa Uganda, wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya nchi yao kupokea wahamiaji kutoka Marekani.
“Kama wahamiaji watakuja, tutaishi nao vizuri tu. Lakini je, Marekani inatusaidia nini katika hili?,” anasema mkazi wa mjini Kampala, Dorcus Kimono.
“Tunataka kusikia kwamba kama nchi yetu itakubali, basi Marekani itajenga barabara au itatusaidia katika sekta za afya na elimu. Hapo itakuwa vizuri.”
Alex Wandeba, mkazi mwingine wa Kampala, haoni sababu ya Uganda kupokea wahamiaji hao. “Uganda ina mzigo mkubwa. Tayari tuna wakimbikizi wengi kutoka nchi jirani. Nadhani sasa inatosha,” anasema.
Eswatini nako hali si shwari juu ya Serikali yake kukubali kupokea wahamiaji kutoka Marekani. Mchambuzi wa siasa, Mphandlana Shongwe, anasema wananchi hawakubaliani na hatua hiyo.
Hasira za wananchi zilikuja baada ya Eswatini kupokea wahamiaji watano, ambao walikuwa na mashitaka ya uhalifu nchini Marekani.
“Hatutaki kuona wahalifu wazoefu wakiingia na kukutana na wahalifu wadogo waliopo hapa nchini,” anasema Shongwe katika mahojiano yake na DW.
Kwa upande mwingine, wanaharakati wa haki za binadamu wanalaani kitendo cha wahamiaji wa Marekani kupelekwa Eswatini.
Ikumbukwe, Taifa hilo la Kusini mwa Afrika lenye watu takribani milioni 1.2, linakabiliwa na shutuma za ukandamizaji wa haki za binadamu.
Wakati huo huo, wanaitaja Sudan Kusini nayo kuwa si sehemu salama kwa wahamiaji kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea kati ya wanajeshi wa Serikali na waasi.
Lakini, kwa mujibu wa Mkuu wa Jukwaa la Asasi za Kiraia kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, Edmund Yakani, Sudan Kusini kukubali kupokea wahamiaji ni njia ya kutafuta ‘huruma’ kutoka kwa Marekani.
“Ni katika kuweka mazingira ya urafiki na utawala wa Rais Trump. Kuna suala la ushuru pia. Huenda Sudan Kusini ikapunguziwa ushuru (wa bidhaa zake zinazozingia Marekani),” anasema.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, alithibitisha kuwa nchi hiyo imekubali kupokea wahamiaji 250.
Pia, mataifa mengine ya Afrika yaliyofikiwa na Marekani yakiombwa kusaini mkataba wa kukubali kupokea wahamiaji ni Liberia, Senegal, Gabon, Mauretania na Guinea-Bissau, ingawa Nigeria imegoma na kusisitiza kuwa ina matatizo mengi ya kukabiliana nayo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img