LONDON, Uingereza
KLABU za Ligi Kuu ya England (EPL) zimeshatumia Pauni bilioni 2.37 katika soko la usajili wa majira haya ya kiangazi, kiasi kikubwa zaidi kuwahi kutumika.
Mkwanja huo umefikia baada ya Leeds United kukamilisha usajili wa straika kutoka AC Milan, Noah Okafor, kwa Pauni milioni 18.
Akisaini mkataba wa miaka minne, nyota huyo raia wa Uswis anakuwa mchezaji wa tisa kusajiliwa na Leeds majira haya ya kiangazi.
Baada ya usajili wa Okafor mwenye umri wa miaka 25, klabu za EPL zilikuwa na rekodi ya kutumia Pauni bilioni 2.36 mwaka 2023.
Kufikia sasa, klabu sita za EPL zimeshavunja rekodi ya usajili, ikiwamo Brentford iliyomnasa Dango Ouattara kwa Pauni milioni 42.5 akitokea Bournemouth.
Burnley nayo ilivunja rekodi yake ya usajili kwa kiungo Lesley Ugochukwu aliyeigharimu kitita cha Pauni milioni 25.
Kwa upande wao, Sunderland nao walivunja rekodi yao ya usajili kwa Pauni milioni 26 zilizotumika kumchukua kiungo raia wa Senegal, Habib Diarra.
Published:


