LISBON, Ureno
KITENDO cha Viktor Gyokeres kushindwa kuungana na wenzake mazoezini akishinikiza kujiunga na Arsenal, kimewatibua mabosi wa klabu yake ya Sporting Lisbon.
Taarifa zinaeleza kuwa uongozi wa Sporting umekerwa na utovu wa nidhamu alioonesha Gyokeres, ambaye alitarajiwa kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Kwa mujibu wa Rais wa klabu hiyo, Frederico Varandas, mshambuliaji huyo atakumbana na adhabu.
Wiki iliyopita, iliripotiwa kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa Arsenal, Andrea Berta, alikuwa Ureno na kufanya mazungumzo na nyota huyo raia wa Sweden.
Gyokeres alikuwa mwiba mchungu kwa mabeki msimu uliopita, ambapo alifunga mabao 54 katika mechi 52.
Washika Bunduki wameshapeleka ofa yao ya Pauni milioni 60 kwa ajili ya Gyokeres mwenye umri wa miaka 27.
Kwa misimu yake miwili klabuni hapo, Gyokeres ameifungia Sporting jumla ya mabao 97 katika mechi 102, akitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu.
Published:


