MADRID, Hispania
KISIWA cha Ibiza. Kinapatikana nchini Hispania na ni moja ya maeneo ghali na yenye starehe za kiwango cha juu duniani.
Kutokana na upekee wake, ni watu maarufu na wenye pesa pekee wanaomudu kukanyaga ardhi ya Ibiza kwa ajili ya kuponda raha.
Sasa, kwa mastaa wa soka wanaokwenda Ibiza, hasa kipindi cha likizo kama hiki cha majira ya kiangazi, jina la Alis Moore si geni kwao.
Kwa nyakati tofauti, aliwahi kuonekana kwenye picha akiwa na Wayne Rooney, Frank Lampard, John Terry, Kieran Trippier, na hivi karibuni ni Jude Bellingham.
Huyu ndiye mrembo anayezitafuna vilivyo pesa za wanasoka wengi barani Ulaya, mara tu wanapofika Ibiza. Anazitafuna vipi?
Bibiye ni Mkurugenzi wa Kampuni iitwayo Faith Concierge, ambayo imekuwa ikiwaandalia kila kitu mastaa wanaotaka kwenda ‘kula bata’ katika Kisiwa hicho.
Kupitia kampuni yake, amekuwa akiwatafutia mastaa vyumba vya kukaa na hata kuwauzia vyakula kwa kipindi chote watakachokuwa pale Ibiza.
Alis anamiliki boti zaidi ya 200, ambazo kwa ile ya bei ya chini kabisa, basi mastaa wamekuwa wakilipa Pauni 1,000 (zaidi ya Sh mil. 3.6 za Tanzania) kwa siku.
Staa wa Manchester City, Jack Grealish, amekwa muhudhuriaji mzuri wa Ibiza, hasa katika eneo maarufu kwa jina la ‘Ocean Beach’, ambako huwa unapigwa muziki, huku vikiuzwa vinywaji vya gharama.
Inaelezwa kuwa staa wa mtandao wa YouTube, KSI, aliwahi kutumia Pauni 51,000 kununua chupa 600 za ‘champagne’ alipotembelea Ocean Beach mwaka 2023.
Ni eneo hilo hilo, ambalo kocha wa Liverpool raia wa Uholanzi, Arne Slot, alionekana akiponda raha siku chache tu baada ya kuiongoza klabu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu ya England (EPL) msimu uliopita.
Katika mahojiano yake na gazeti la Mail Sport, Alis anasema: “Huwa pia tunakodisha magari ya bei mbaya kama Ferrari na Lamborghini.
“Lakini hapa Ibiza wachezaji huwa wanapenda kuja wakiwa kundi, hivyo magari aina ya G-wagon na Range Rover ndiyo maarufu zaidi.”
Kwa upande wa usalama wa wateja, Alis anasema huwa wanakodisha pia ulinzi binafsi endapo mchezaji atahitaji.


