CAIRO, Misri
FAINALI za Mataifa Afrika kwa upande wa soka la Wanawake (WAFCON) zitaanza kutimua vumbi wikiendi hii (Julai 5) huko Morocco.
Wenyeji kwa mara ya pili mfululizo, Morocco, watakata utepe kwa kuvaana na Zambia, mchezo utakaochezwa katika Uwanja wa Olimpiki mjini Rabat.
Nigeria, timu pekee iliyotwaa ubingwa mara nyingi (9), itatupa karata yake ya kwanza kwa kuikabili Tunisia.
Mabingwa watetezi, Afrika Kusini, wao wataanza safari ya kutetea taji lao kwa kuikabili Ghana. ‘Sauzi’ walibeba ubingwa mwaka 2022.
Timu shiriki ni 12, ambapo zimegawiwa katika makundi matatu. Kila kundi lina timu nne.
Kundi A: Morocco, Zambia, Senegal, DRC. Kundi B: Nigeria, Tunisia, Algeria na Botswana. Kundi C: Afrika Kusini, Ghana, Mali na Tanzania.
Kati ya timu 12 zitakazoshiriki, ni Nigeria na Afrika Kusini pekee zilizowahi kutwaa taji la michuano hiyo.
Kwa upande wa miundombinu, viwanja sita katika miji mitano vitatumika kwa ajili ya fainali hizo.
Ifahamike pia, kwamba viwanja viwili kati ya hivyo vinapatikana jijini Casablanca.
Uwanja mkubwa zaidi ni Larbi Zaouli, ambao uko Casablanca na unapokea mashabiki 30,000.
Viwanja vingine na idadi ya mashabiki ni kama ifuatavyo;
Olimpiki (21,000), Honneur (19,800), El Bachir (15,000), Berkane (15,000) na Pere Jego (10,000).


