25.1 C
New York

Madaktari bingwa 50 waweka kambi Singida

Published:

Na Mwandishi wetu, Gazetini

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dk. Fatma Mganga amewapokea madaktari bingwa na bingwa bobezi 50 wa Rais Samia na kuwataka kuwahudumia watanzania wa mkoa huo kwa moyo wa upendo ili kuacha kumbukumbu wakiondoka.

Dk. Mganga amesema hayo Aprili 28, 2025, wakati wa mapokezi ya madaktari hao watakaofanya kazi za kibingwa na ubingwa bobezi katika halmashauri saba  za mkoa huo, sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wa afya waliopo katika ngazi za msingi.

“Kambi ya mwaka jana ilifanikiwa kwa kiwango kikubwa, ambapo maelfu ya wananchi walihudumiwa kwa weledi na ufanisi. Mwaka huu tumejipanga kuvuka mafanikio hayo, kwa kutoa huduma bora zaidi na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” amesema Dk. Mganga.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa maono yake katika kuboresha sekta ya afya. Wananchi tuendelee kuiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kutafuta afya bora kwa wote. Pia nawapongeza watumishi wa sekta hii kwa kazi yenu ngumu ya kuwahudumia wananchi,” ameongeza.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kufika hospitalini hapo kupata huduma hizo za kibingwa, akisisitiza kuwa fursa hiyo ni adimu na kwamba madaktari hao wanakuja mara chache, hivyo ni muhimu kuitumia ipasavyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Programu ya Uzazi Salama Wizara ya Afya, Dk. Phineas Sospeter, amesema kambi hiyo inatoa fursa kwa wananchi, hususan wale wanaoishi katika maeneo ya Singida na mikoa jirani, kupata huduma za kibingwa bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Dk. Phineas Sospeter amesisitiza kuwa Rais  Samia ameona umuhimu wa kuwafikia wananchi katika ngazi za chini, ambazo mara nyingi hukosa huduma hizo muhimu ambapo madaktari hao watakuwepo hadi Mei 3,2025.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img