11.3 C
New York

TACAIDS yahimizwa kuongeza kasi ya huduma za VVU na UKIMWI kwa jamii za wavuvi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeitaka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu, huduma za kinga, matibabu na matunzo kwa wavuvi wanaoishi katika maeneo ya maziwa na bahari.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akizungumza na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu namna  Wizara yake inavyo tekeleza kuhusu hatau za ujumuishi wa afua za VVU na UKIMWI kwenye sekta ya UVUVI kilichofanyikaOktoba 22,2024 Bungeni Dodoma.

Hii ni baada ya kubaini kuwa kiwango cha elimu ya kujikinga na VVU miongoni mwa wavuvi bado ni cha chini, huku upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI ukiendelea kutokidhi viwango vya kuridhisha.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika leo Oktoba 22, 2024 Bungeni jijini Dodoma, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Christina Mzava, alisema maambukizi ya VVU kwa wavuvi bado ni tatizo kubwa, ambapo kiwango cha maambukizi kipo juu kwa asilimia 7, ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa.

Amesisitiza kuwa TACAIDS inahitaji kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu na huduma katika maeneo ya mialo ili kukabiliana na hali hiyo.

“Lazima tuongeze kasi katika kutoa elimu ya kujikinga na VVU, pamoja na huduma za kinga, matibabu, na matunzo kwa jamii za wavuvi, ambao kwa sasa wanakabiliwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU. TACAIDS inakazi kubwa ya kuhakikisha huduma hizi zinawafikia kwa ufanisi wavuvi walio kwenye maziwa na bahari,” amesema Dk. Mzava.

Wajibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Katika kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Samweli Mwashamba, aliwasilisha taarifa kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega. Amesema Wizara hiyo inaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za VVU, UKIMWI, na magonjwa sugu yasiyoambukiza kwa mujibu wa waraka wa Utumishi wa Umma wa mwaka 2014.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Afya na Masuala ya UKIMWI Dk. Christine Mzava akizungumzia umuhimu wa kuongeza Afua za UKIMWI katika jamii ya Wavuvi maeneo ya Bahari na Maziwa wakati wa kikao cha kamati hiyo, kilichofanyika Bungeni Oktoba 22,2024.

Mwashamba alieleza kuwa hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na ujumuishaji wa masuala ya VVU na UKIMWI katika sera ya Uvuvi ya mwaka 2015, kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa afua hizo, pamoja na utoaji wa lishe, elimu, na upimaji wa hiari kwa watumishi wa Wizara na wavuvi.

“Wizara pia imeanzisha vituo vya upimaji na ushauri nasaha kwa wavuvi, huku ikisambaza makasha 30 ya kuhifadhia kondomu na kondomu 334,872 kwenye maeneo ya kazi ya Wizara katika kipindi cha mwaka 2023/24,” ameongeza Mwashamba.

Changamoto za maambukizi kwa wavuvi

Mwashamba amebainisha kuwa sababu kuu zinazochangia kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU kwa wavuvi ni pamoja na matumizi yasiyosahihi ya kondomu, imani potofu juu ya matumizi ya kondomu, na uelewa mdogo kuhusu VVU na UKIMWI.

Kamati ya Kidumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Mhina  wakifuatilia ufafanuzi wa taarifa  kuhusu utekelezaji wa hatua za ujumuishi wa Afua za VVU na UKIMWI kwenye sekta ya UVUVI, Oktoba 22,2024.

Hali hiyo imechangiwa zaidi na upatikanaji hafifu wa huduma za afya katika maeneo ya mialo, hususan kwenye visiwa.

Amesema kuwa juhudi zaidi zinahitajika katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika mialo, kwani asilimia 51 ya huduma hizo zinapatikana katika mialo 1307 pekee. Pia, aliainisha kuwa sensa za wavuvi zinaendelea ili kuweka mikakati bora ya utoaji wa huduma hizo.

Elimu na huduma kwa watumishi wa Wizara

Katika kipindi cha mwaka 2023/24, jumla ya watumishi 387 wa Wizara walipatiwa elimu ya VVU na UKIMWI pamoja na ushauri nasaha na vipimo. Aidha, Wizara ilitoa lishe na nauli kwa watumishi waliojulikana kuishi na VVU ili kusaidia afya na ustawi wao.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Mhina akitoa ufafanuzi kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI juu ya namna Wizara ya Mifugo na Uvuvi inavyotoa huduma za VVU na UKIMWI kwa watumishi wa Wizara ya Uvuvi na Mifugo.

Kamati hiyo ya Bunge ilihitimisha kwa kuhimiza TACAIDS kushirikiana zaidi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuongeza nguvu za kutoa huduma bora za VVU na UKIMWI kwa jamii za wavuvi ili kupunguza kiwango cha maambukizi kwenye sekta hiyo muhimu.

Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Samweli Mwashamba, akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa niaba ya Waziri kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI jijini Dodoma Oktoba 22, 2024.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img