18.2 C
New York

Wananchi Kishapu walia umbali wa maji, shule

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WANANCHI wa Kata ya Ndoleleji katika kijiji cha Mwalata wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wameeleza wanavyotembea umbali wa zaidi ya kilometa sita kupata maji safi, wakisema changamoto hiyo imekuwa ikiathiri shughuli zingine za kiuchumi.

Sambamba na hilo, pia wakazi wa eneo hilo wamefichua changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya Kilometa 12 kuifuata shule ya Sekondari ya Mangu.

Hayo yamezungumzwa jana Novemba 4, 2026 katika mkutano wa wananchi na Mwenyekiti wa Halmashuri ya Wilaya ya Kishapu, Josephat Limbe, walipokuwa wakitoa changamoto zinazowakabili.

Mkazi wa Kijiji cha Mwalata, Gaudencia Jisandu, amesema: “Changamoto ya maji imekuwa mzigo mkubwa tunatembea zaidi ya kilometa sita kufuata maji ya Mto Tungu. Tunaomba Halmashuari kutusaidia kuharakisha upatikanaji wa maji safi.

“Wanawake tunalazimika kuamka mapema na kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali inayotuathiri katika shughuli za kiuchumi na ustawi wa familia,” amesema.

Naye Lenisi Jishanga Zengo ameibua changamoto ya umbali wa shule ya Sekondari Mangu, ambapo wanafunzi hutembea zaidi ya kilometa 12 kuhudhuria masomo

Wakati huo huo, ameeleza uchakavu wa majengo ya Shule ya Msingi Mwalata yaliyojengwa mwaka 1995, yakiwemo madarasa sita na ofisi moja ambayo yanahitaji ukarabati kutokana na uchakavu wake.

“Licha ya changamoto hiyo, shule imeendelea kufanya jitihada kwa kutumia mapato yake ya ndani, ambapo imejenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja na sasa imefikia hatua ya kukamilisha boma,” amesema Zengo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Limbe, amesema tayari wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilayani Kishapu umepitisha bajeti ya Shilingi milioni 50 katika Mwaka wa Fedha 2026/2027 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu na kuweka miundombinu ya maji.

“Ndugu zangu wananchi wa Mwalata, nikiri kabisa kuwepo kwa tatizo la ukosekanaji wa maji safi katika eneo letu ila RUWASA bado inasubiri kuletewa fedha hizo na kisha zikifika zitatumika.

“Mradi huo unatarajiwa kujumuisha ufungaji wa umeme wa jua, pamoja na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji, hatua itakayosaidia kupunguza adha mnayoipata,” amesema Limbe.

Kuhusu changamoto ya umbali wa wanafunzi kwenda shule, Limbe amesema Halmashauri kupitia vikao vya Serikali za Vijiji (VDC) imepitisha azimio la kujenga shule Shikizi ya Sekondari katika Kijiji cha Masanga ndani ya mwaka wa fedha 2026/2027, hatua itaondoa changamoto iliyopo.

Related articles

Recent articles