Na Faraja Mulugu, Gazetini
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limewaomba radhi wateja wake katika maeneo ya Mbagala, Kigamboni, Mkuranga na Kibiti kutokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya umeme iliyotokana na hitilafu ya kebo ya ardhini ya msongo wa kilovolti 132 katika eneo la Gongo la Mboto, Dar es Salaam.
Akizungumza leo, Alhamisi, Novemba 5, 2026, alipotembelea eneo lilipotokea hitilafu hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowelle, amesema hitilafu hiyo ilitokea Novemba 3, mwaka huu na kuathiri njia inayosafirisha umeme kwenda katika vituo vya kupoza umeme vya Mbagala na Dege.
Gowelle, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, amewaomba radhi wateja walioathirika na changamoto hiyo, huku akiwashukuru kwa uvumilivu wao wakati shirika likiendelea na jitihada za kurejesha huduma katika hali ya kawaida.
Amesema baada ya kubaini hitilafu hiyo, Tanesco ilichukua hatua za haraka kwa kuwahamishia wateja katika njia mbadala ili waendelee kupata huduma wakati wataalamu wakishughulikia tatizo katika njia ya ardhini.
“Tulichukua hatua za haraka za kuweza kurekebisha hali hiyo kwa kuwahamishia wateja katika njia mbadala ili waweze kuendelea kupata huduma wakati wataalamu wakiendelea kushughulikia changamoto ambayo imejitokeza katika laini hii ya ardhini,” amesema Gowelle.

Amesema pamoja na hatua hiyo, baadhi ya maeneo yameendelea kukumbwa na changamoto ya umeme kusuasua, hasa wakati wa mchana, kutokana na njia mbadala kutokuwa na uwezo wa kubeba mahitaji yote ya umeme kwa wakati mmoja.
“Njia ambayo wamehamishiwa kwenye njia mbadala inakuwa haina uwezo wa kubeba mahitaji yote hayo kwa wakati mmoja,” amesema.
Ameongeza kuwa shirika linaendelea na matengenezo ya kebo hiyo na kuwaomba wateja waendelee kuwa na uvumilivu hadi huduma itakaporejea katika hali yake ya kawaida.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco anayeshughulikia Usafirishaji Umeme, Mhandisi Zakaria Mgalama, amesema hitilafu hiyo imetokea katika njia ya msongo wa kilovolti 132 inayosafirisha umeme kutoka kituo cha Gongo la Mboto kwenda katika vituo vya kupoza umeme vya Mbagala na Dege.
Amesema njia hiyo inahudumia maeneo ya kusini mwa Jiji la Dar es Salaam, yakiwemo Mbagala na Kigamboni, pamoja na maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani.
Mgalama amesema baada ya hitilafu kutokea Novemba 3, wataalamu waliweza kuhamishia wateja katika njia mbadala, lakini njia hiyo ina uwezo mdogo ukilinganisha na ile iliyopata hitilafu.
“Tunapokuwa kwenye mahitaji ya juu ya mchana tunajikuta tunalazimika baadhi ya maeneo machache kupunguza kidogo ili kuweza kuhimili kutokana na uwezo wa njia hiyo. Lakini inapofika usiku basi wateja wote wanarudishiwa na kupata umeme,” amesema.
Ameongeza, Tanesco inaendelea na jitihada za kutatua changamoto hiyo na inatarajia ndani ya siku chache zijazo huduma kurejea katika hali ya kawaida.
Aidha, Mgalama amesema Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya umeme itakayosaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma katika maeneo hayo.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Mkuranga na mradi wa kilovolti 220 kutoka Pugu kuelekea Undani, ambayo inalenga kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme na kusaidia maeneo ya kusini mwa Dar es Salaam.
Akijibu swali kuhusu iwapo hitilafu za aina hiyo zimewahi kutokea hapo awali na muda unaohitajika kuzitatua, Mgalama amesema matatizo katika nyaya za umeme zinazopita chini ya ardhi yamewahi kutokea, lakini muda wa matengenezo hutegemea ukubwa wa hitilafu na eneo ilipotokea.
Amefafanua kuwa tofauti na nyaya zinazopita juu ya ardhi, nyaya za chini ya ardhi huhitaji muda zaidi wa matengenezo, hasa pale hitilafu inapokuwa katikati ya njia na kulazimu uchimbaji ili kufikia sehemu iliyoathirika.
Hata hivyo, alisema muda kamili wa kurekebisha hitilafu ya sasa utajulikana baada ya wataalamu kukamilisha uchunguzi wa kina.


