3.2 C
New York

Dk. Biteko ahimiza Uhifadhi wa Viumbe vya Baharini na Mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amewataka Watanzania kulinda viumbe vya baharini na kuhifadhi mazingira ya bahari kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Dk. Biteko alitoa wito huo leo, Julai 4, 2024, wakati akifungua Kongamano la Tatu la Uchumi wa Buluu lenye kaulimbiu: “Kuunganisha Usalama Baharini, Utunzaji wa Mazingira na Maendeleo ya Teknolojia kwa ajili ya Ukuzaji wa Uchumi wa Buluu.”

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

“Tunapofanya majadiliano leo, tujikite kwenye kanuni za uendelevu, usawa, na uvumbuzi ili kongamano hili liwe mwanga unaotuongoza kwenye uchumi wa buluu unaoinua jamii zetu. Ninawasihi kila mmoja wenu ashiriki kikamilifu ili tuweze kupata matokeo chanya,” alisema Dkt. Biteko.

Dk. Biteko alisema uchumi wa buluu unatambuliwa kama mchangiaji mkubwa wa maendeleo endelevu ambapo jamii hutumia rasilimali za bahari kwa njia endelevu na zinazozingatia uhifadhi wa mazingira.

“Pia, uchumi wa buluu huchochea uvumbuzi wa fursa kama vile teknolojia ya kibayoteknolojia na nishati ya bahari, kutoa suluhu za nishati mbadala na tiba, kusaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia ulinzi wa mifumo ikolojia, na kuhakikisha usalama wa usafiri wa majini na kuzuia shughuli haramu baharini,” aliongeza Dk. Biteko.

Hata hivyo, Dk. Biteko alibainisha kuwa uchumi wa buluu unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo uvuvi wa kupita kiasi, uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya hali ya hewa, uvuvi haramu, uharibifu wa makazi, na ukosefu wa taarifa sahihi. Aliweka wazi kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto hizo kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani.

Dk. Biteko pia alieleza kuwa mwaka 1991 Tanzania ilianzisha Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ambacho kinashirikiana na vyuo vingine kufanya tafiti, kubadilishana wataalam, na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa serikali, watu binafsi, na wadau wengine kuhusu maswala ya bahari.

“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ibara ya 136 (e) imeelekeza kuibua na kuendeleza sekta mpya za uchumi ikiwemo uchumi wa buluu, ubunifu, na uchumi wa kidigitali. Uchumi wa buluu ni shughuli zote za kiuchumi zinazohusiana na bahari na maziwa makuu pamoja na rasilimali zake,” alisisitiza Dk. Biteko.

Naye, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema uchumi wa buluu ni uchumi mtambuka unaohusisha sekta mbalimbali. Alisema kongamano hilo limekuwa chachu katika kutoa fursa na mafunzo kwa Watanzania katika sekta ya bahari.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema mkoa huo unahusika kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa buluu na alihimiza wadau kuendelea kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img