21 C
New York

Kamati yaridhishwa namna Magereza Chato linavyotekeleza mwitikio wa UKIMWI

Published:

Na Nadhifa Omar, Chato

Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imetembelea Gereza la Wilaya ya Chato kwa lengo la kujionea namna mwitikio wa UKIMWI unavyotekelezwa katika gereza hilo ambapo wamekutana na mahabusu, wafungwa, askari, maafisa pamoja watumishi wa umma.

Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Stanslaus Nyongo amesema kamati imeridhishwa na jinsi Magereza inavyopanga na kutekeleza mikakati ya Mwitikio wa UKIMWI katika gereza hizo.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa afua za Mwitikio wa UKIMWI katika gereza la Chato zinaridhisha na pongezi nyingi zimwendee Mkuu wa jeshi la Magereza kwani kwa sasa hakuna malalamiko, pia shukrani zimwendee, Samia Suluhu Hassan kwani kila kinachofanyika ni kutokana na mwongozo na maelekezo yake.

Aidha, amewasisitizia kuchukua tahadhari ya maambukizi ya VVU ikiwa ni pamoja na kupima afya kwa wale ambao hawajapima ili wajue afya zao,  pamoja na kuanzishiwa dawa kwa wale ambao watagundulika kuwa na maambukizi ya VVU.

Amewasisitizia kuwa kupima na kuanza dawa mapema kuna faida ikiwa ni pamoja na kuimarisha afya, na kutoendelea kuwaambukiza mtu mwingine endapo mko kwenye mahusiano ya kingono.

Ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia TACAIDS kuangalia namna ambavyo itaandaa mkakati maalum wa kutekeleza afua za UKIMWI katika magereza yote nchini ikiwa ni pamoja na kuwajenga uwezo maafisa magereza katika utoaji elimu ya VVU katika maeneo yao.

“Niombe Ofisi ya Waziri Mkuu kama Mratibu wa masuala ya UKIMWI muangalie namna mtakavyo kuwa na mkakati wa kutekeleza afua za UKIMWI katika magereza nchini na kufanya magereza kuwa mkoa wa kimkakati,ili kuhakikisha maambukizi ya VVU yanapungua pamoja na kuwawezesha Afisa Magereza kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU”.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe Ummy Nderiananga akizungumza katika ziara hiyo amesema Ofisi ya Waziri Mkuu inapokea maagizo yote yanayotolewa na Kamati hiyo kwa ajili ya Utekelezaji.

Aidha, amelipongeza jeshi la Magereza kwa kuendelea kutekeleza afua za Mwitikio wa UKIMWI,pamoja na kuweka mikakati mizuri ambayo inalenga  kumaliza UKIMWI ifikapo 2030.

Kamati ilikutana na Mahabusu na Wafungwa, katika risala yao wamebainisha changamoto ambazo ni ukosefu wa dawa za kukidhi mahitaji, maji, upungufu wa magodoro na blanketi kutokana na ongezeko la mahabusu pamoja usafiri.

Kamishina Msaidizi wa Magereza Dk. Richard Mwankina alisema kuwa elimu ya afya kuhusu VVU na UKIMWI hutolewa na watumishi wa afya waliopo gereza Chato kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya, ambapo wafungwa na mahabusu wamekuwa wakifundishwa namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU na magonjwa ya ngono lakini pia wasiawaambukize wengine .

Ameongeza kuwa wafungwa na mahabusu wanapata habari na mafunzo mbalimbali wakiwa katika gerezani kupitia televisheni na vipeperushi ili kuongezea uelewa zaidi.

Aidha, Dk. Mwankina alisema kuwa kwa sasa jumla ya wafungwa na mahabusu 24 ndio wanaotumia dawa (ARV)

Awali kamati ilitembelea hospitali ya rufaa ya Kanda ya Chato ambapo katika hospital hiyo pamoja na huduma nyingine inatoa huduma za tiba na matunzo kwa Watu Wanaoishi na VVU ambazo hutolewa kwa siku tano katika wiki kwa ajili ya kutoa dawa ,kuchukua vipimo ,ushauri na huduma nyingine,upimaji wa VVU,upimaji wa kiwango cha maambukizi ya VVU pamoja na huduma kwa wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia.

Taarifa ya hospitali hiyo imeonesha kuwa katika mwaka 2023 jumla ya wateja 1,253 walipima VVU ambapo wanaume walikuwa 682na wanawake 571, jumla ya watu 21 walibainika kuwa na maambukizi ya VVU. Aidha, hospitali inaendelea kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU kwa kuhamasisha matumizi sahihi na endelevu ya kondomu kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Afya na masuala ya UKIMWI, Stanslaus Nyongo amepongeza jitihada zinazofanyika katika kuimarisha huduma za afya na kuagiza fedha za miradi zinazotengwa zitolewe ili miradi inayoanzishwa isikwame.

Mwenyekiti alielekeza Serikali kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya Afya zitolewe kwa wakati ili miradi hiyo isikwame, uwekezaji huu ni mkubwa sana katika hospitali hii ya rufaa ya kanda ya Chato kwa kuwa itapunguza mzigo kwa hospitali ya moyo ya Jakaya Kikwete Dar es Salaam.

Alisisitiza baada ya kukamilika kwa hospitali hii haitarajiwi kuwa kuna mtu wa Kanda ya Ziwa atakwenda JKCI kupata huduma, kwa kuwa huduma zote zitapatikana hapa” alisema Mhe Nyongo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img