Na mwandishi wetu, Gazetini-Dar
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeanza mchakato wa kupitia upya bei za Gesi Asilia Iliyokandamizwa (CNG) inayotumika kwenye magari, baada ya kubainika kuwa viwango vya sasa vimeendelea kutumika kwa takribani miaka 15 bila kufanyiwa marekebisho.
Mapitio hayo yanalenga kuweka mfumo wa bei unaozingatia gharama halisi za uendeshaji, viwango vya faida kwa watoa huduma na uwezo wa wananchi kumudu gharama za nishati hiyo.
Mchakato huo pia utazingatia mabadiliko ya gharama katika mnyororo mzima wa huduma za CNG, ikiwemo uzalishaji, usafirishaji, uhifadhi na usambazaji wa gesi asilia.
Akizungumza leo, Novemba 23, 2026, jijini Dar es Salaam, katika semina ya wadau kuhusu usalama wa matumizi ya CNG, Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Mhandisi Lorivii Lon’gidu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Salum Mnuna, amesema wameanza kukusanya maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya viwango vya faida na bei kikomo za nishati hiyo.
“Tunapenda kuona maoni yenu na ushauri wenu kuhusu mapendekezo ya viwango vya faida na bei kikomo za CNG, ili sisi kama wadhibiti tuyazingatie na kuhakikisha shughuli hizi zinafanikiwa kwa njia salama zaidi,” amesema.
Amesema ushirikishwaji wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha maamuzi yatakayofikiwa yanazingatia maslahi ya wawekezaji, watoa huduma na wananchi wanaotumia nishati hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mitambo ya Gesi Asilia (CNG) wa EWURA, Selemani Chombo, amesema mapitio hayo yanazingatia gharama za uendeshaji, mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni pamoja na gharama za kusafirisha gesi kutoka kwenye vyanzo vya uzalishaji hadi maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kwa sasa kilo moja ya CNG inauzwa kwa Sh 1,550 jijini Dar es Salaam, lakini ongezeko la matumizi ya nishati hiyo na upanuzi wa huduma katika maeneo ya Morogoro, Kibaha, Mtwara na Ruvuma
umeongeza umuhimu wa kuwa na mfumo wa bei unaozingatia gharama halisi za utoaji wa huduma katika kila eneo.
Ameeleza kuwa EWURA itazingatia sheria na kanuni zilizopo katika mchakato huo, huku wazalishaji, watoa huduma na watumiaji wakipewa nafasi ya kutoa maoni kabla ya viwango vipya vya bei kutangazwa na kuanza kutumika rasmi.


