NEW YORK, Marekani
BODI ya Wakurugenzi ya kampuni ya teknolojia ya Nvidia imepiga kura kwa kauli moja kumrejesha Jensen Huang katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji (CEO), ikieleza kuwa ina imani naye kuendelea kuiongoza kampuni hiyo.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Nvidia, Mwenyekiti wa Bodi amesema uamuzi huo umefikiwa kwa makubaliano ya wajumbe wote, akibainisha kuwa kurejea kwa Huang ni kwa manufaa ya wanahisa, wafanyakazi, washirika na wateja wa kampuni hiyo.
Akizungumzia kurejea kwake, Huang amesema anapokea jukumu hilo kwa heshima kubwa, unyenyekevu na dhamira mpya ya kuendelea kuiongoza Nvidia, ambayo ameielezea kuwa miongoni mwa taasisi muhimu zaidi za teknolojia duniani katika kipindi hiki cha mapinduzi mapya ya viwanda.
Ametoa shukrani kwa Bodi ya Wakurugenzi kwa kumwamini tena, huku akimtaja Mwenyekiti Harvey Jones kwa uongozi wake, pamoja na Colette Kress na timu ya viongozi waandamizi kwa kusimamia shughuli za kampuni hiyo katika kipindi hicho.
Aidha, amewashukuru wafanyakazi, wanahisa, viongozi wa sekta ya teknolojia na washirika wa Nvidia kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa kumuunga mkono wakati wote.
Huang pia ameitaja familia yake kuwa nguzo muhimu ya upendo na msaada katika kipindi hicho, akisema ana shauku kubwa ya kurejea kazini na kuendelea na majukumu yake.
“Ninashukuru zaidi kwa upendo na msaada wa familia yangu. Nina shauku kubwa ya kurejea kazini,” amesema Huang.


