LONDON, Uingereza
HIVI karibuni, Antonio Conte alisema klabu inayohitaji makombe haiwezi kuacha kumpa ajira. Ulikuwa ni ujumbe maalumu kwa mabosi wa Manchester United.
Kwa miaka mingi, Conte amekuwa akihusishwa na klabu hiyo lakini haikuwahi kutokea kupewa kazi. Ilianzia pale Alex Ferguson alipostaafu mwaka 2013.
Wakati huo Ferguson anaachia ngazi, Conte alikuwa mmoja ya makocha wanaofanya vizuri akiwa kwenye benchi la ufundi la Juventus.
Alikuwa ameiongoza Juventus kutwaa taji la Serie A bila kufungwa katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo. Ripoti nyingi zikamuhusisha kuchukua mikoba ya Ferguson pale Old Trafford.
Hata hivyo, dili halikutokea, na badala yake mabosi wa Man United waliamua kumpa ajira David Moyes, ingawa pia zipo stori kwamba Jose Mourinho ndiye aliyekuwa akitakiwa lakini aligoma na kurudi zake Chelsea.
Conte akalazimika kubaki Turin na kuiwezesha Juventus kutwaa taji la Ligi [Serie A] msimu uliofuata.
Mwaka 2014, jina la Conte likaibuka tena Old Trafford. Ni baada ya klabu hiyo kumtimua Moyes akiwa amefanya kazi kwa miezi 10 pekee, wakati huo Man United ikiwa nafasi ya saba kwenye msimamo.
Wakati Conte anatajwa kwenda Old Trafford, tayari alikuwa akielekea mwishoni mwa mkataba wake na Juventus. Makocha wengine waliokuwa wakihusishwa na Man United ni Louis van Gaal, Carlo Ancelotti na Diego Simeone.
Safari hii, licha ya kukutana na kufanya mazungumzo na mabosi wa Man United, Conte ‘alipotezewa’ na Van Gaal akaajiriwa. Conte akaenda kuinoa timu ya soka ya Taifa ya Italia.
Hata ilipotokea Van Gaal akatimuliwa mwaka 2016, mabosi wa Man United waliamua kwa mara nyingine ‘kumfungia vioo’ Conte. Mwezi mmoja baada ya Muitalia huyo kuajiriwa Chelsea, wao wakamtangaza Mourinho ‘Special One’.
Mwaka 2018, Mourinho akiwa ameshatimuliwa baada ya kufanya kazi, jina la Conte lilihusishwa tena na Man United. Wakati huo, naye alishaondoka Stamford Bridge, hivyo ilikuwa rahisi.
Kwa mara nyingine, Man United hawakuona umuhimu wa kumchukua, na badala yake walimgeukia Ole Gunnar Solskjaer, ambaye hata hivyo alifungashiwa virago mwaka 2021.
Conte, kama kawaida, akahusishwa kwenda Old Trafford. Ni wakati ambao hakuwa na timu baada ya kuondoka Iner Milan aliyokuwa ameipa taji la kwanza la Serie A baada ya ukame wa miaka 11.
Lakini, Conte alikumbana na changamoto ya kupingwa na baadhi ya wakongwe wa Man United, akiwamo beki wa kulia wa zamani wa timu hiyo, Garry Neville.
“Conte anapatikana kwa sasa lakini kama ningekuwa mimi nisingemleta Manchester United. Nisingemleta. Sidhani kama Antonio Conte ni kocha sahihi kwa Manchester United,” alisema Neville.
Mbaya zaidi, aliyekuwa staa wa Man United kipindi hicho, Cristiano Ronaldo, naye alipinga ujio wa Conte akisema mbinu zake za ufundishaji haziwezi kuisaidia timu hiyo.
Tangu hapo, Man United imeshapita chini ya makocha wengi, wakiwamo Ralf Rangnick, Erik ten Hag, Ralf Rangnick, Ruben Amorim, Michael Carrick, na sasa Pochettino.
Kwamba ndani ya miaka 13 tangu Ferguson alipostaafu, Man United, licha ya kuajiri makocha nane tofauti, haijawahi kutwaa taji la Ligi Kuu ya England. Conte alibeba moja akiwa na Chelsea [2016-17].


