Na mwandishi wetum Gazetini-Arusha
KAMPUNI ya Mbolea ya Mijingu (Mjingu Mining and Fertilizer Limited) imeeleza kuwa imewekeza katika uzalishaji wa mbolea zenye mchanganyiko wa virutubisho muhimu kwa ajili ya kuboresha afya ya udongo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya bustani, ikiwemo mboga mboga.
Hatua hiyo inalenga kuwasaidia wakulima kupata mazao bora na kuongeza tija, huku wakitumia mbolea zinazozingatia mahitaji halisi ya udongo wa Tanzania.
Akizungumza katika maonesho ya kilimo ya Hortilogistica yaliyofanyika Arusha, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Kisuma Mapunda, amesema mbolea zao zimeonesha matokeo mazuri katika uzalishaji wa mboga mbalimbali, ikiwemo bamia na pilipili hoho.
Amesema mafanikio hayo yameonekana pia katika mashamba yaliyopo Tengeru, ambako wakulima wametumia mbolea za kampuni hiyo katika uzalishaji wa mazao hayo na kupata matokeo mazuri.
Amesema kampuni hiyo ina aina saba za mbolea zinazokidhi mahitaji tofauti ya wakulima, zikiwemo za kupandia na kukuzia, huku nyingine ikiwa na virutubisho nane muhimu kwa ukuaji wa mimea.
Amesema virutubisho hivyo vinavyosaidia kuboresha afya ya udongo na kuipa mimea lishe inayohitajika na kuwa nyingine ina virutubisho nane na imeonesha kufanya vizuri katika kilimo cha mboga mboga.
Mapunda amesema ubora wa bidhaa hizo unatokana na tafiti zilizofanyika kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ili kuhakikisha mbolea zinazozalishwa zinakidhi mahitaji ya udongo na wakulima wa Tanzania.
Amesema pamoja na ubora wa bidhaa hizo, kampuni imezingatia pia uwezo wa mkulima kuzipata kwa bei nafuu kupitia mpango wa ruzuku ya Serikali.
Ameongeza kuwa kampuni ina magari 24 ya kusambaza mbolea katika mikoa mbalimbali nchini na mtandao wa mawakala zaidi ya 500, hali inayorahisisha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa wakulima.
Katika kuhakikisha wakulima wanapata matokeo yanayotarajiwa, amesema kampuni imeanzisha mashamba darasa ya mboga mboga katika maeneo mbalimbali nchini, ambako wakulima wanaweza kujionea matokeo ya matumizi ya mbolea hizo.
Pia, kampuni ina wataalamu wa kilimo wanaowatembelea wakulima na kuwapatia elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji na kulinda afya ya udongo.


