Na Editha William, Gazetini – Kagera
Timu ya Omukishenye FC imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Musila FC katika mchezo wa kirafiki uliochezwa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Ligi ya Diwani wa Kata ya Hamgembe, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera.
Omukishenye FC, inayopatikana katika Kata ya Hamgembe, imepata ushindi huo dhidi ya Musila FC kutoka Kisiwa cha Musila, huku ikijiandaa na mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Novemba 10, 2026.
Ligi hiyo inadhaminiwa na Diwani wa Kata ya Hamgembe, Muhaji Kachwamba Abubakari, ambapo katika mchezo wa ufunguzi Omukishenye FC itakutana na Furniture FC.
Akizungumza baada ya mchezo huo, nahodha wa Omukishenye FC, Cyprian Ephraim, amesema ushindi huo ni sehemu ya maandalizi ya timu hiyo kuelekea kwenye ligi, huku wakilenga kuanza mashindano kwa matokeo mazuri.
Aidha, amewataka mashabiki na wapenzi wa soka kujitokeza kwa wingi Novemba 10, 2026, kuishangilia timu hiyo katika mchezo wake wa ufunguzi dhidi ya Furniture FC.
Amesema sapoti ya mashabiki itakuwa chachu kwa wachezaji katika kupambana na kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo.


