Na mwandishi wetum Gazetini-Dodoma
BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendesha mafunzo ya kuimarisha usimamizi wa fedha za umma katika sekta ya afya, yakilenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya huduma za afya.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo Novemba 11, 2026, jijini Dodoma na yanatarajiwa kuhitimishwa kesho, Novemba 12, yakishirikisha wahasibu, wakaguzi wa ndani na nje pamoja na wataalamu wengine wa sekta hiyo.
Akifungua mafunzo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia masuala ya afya, Prof. Tumaini Nagu, amesema Serikali imetenga Sh bilioni 626 kwa ajili ya sekta ya afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hivyo kunahitajika usimamizi madhubuti ili fedha hizo zilete matokeo yaliyokusudiwa.
“Tunatambua kuwa rasilimali ni chache, hivyo kila shilingi inayotengwa kwa ajili ya afya lazima isimamiwe vizuri, itumike kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma za afya,” amesema Prof. Nagu.
Amesema mafunzo hayo yataimarisha mifumo ya udhibiti wa fedha, kupunguza mianya ya upotevu wa fedha na vifaa tiba, pamoja na kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa I. Mzenzi, amesema wahasibu na wakaguzi wana wajibu muhimu wa kuhakikisha fedha za sekta ya afya zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa wahasibu katika usimamizi wa malipo, wakaguzi wa ndani katika kuchunguza mifumo ya udhibiti na utawala, na wakaguzi wa nje katika kutathmini taarifa za fedha.
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa NBAA, Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mfuko wa Global Fund, Shirikisho la Wahasibu Afrika (PAFA) na Shirikisho la Kimataifa la Wahasibu (IFAC).
Washiriki wametakiwa kutumia maarifa watakayoyapata kuimarisha uwajibikaji na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


