Na Christopher Msekena, Gazetini
STAA wa muziki wa Injili nchini Tanzania, Japhet Zabron, amesema amefurahishwa na sapoti aliyoipata kutoka kwa Charlene Ruto, mtoto wa Rais wa Kenya, William Ruto, ambaye hivi karibuni alifunga ndoa na Mtanzania Isaya Yunge jijini Mwanza.
Charlene ameonesha sapoti hiyo kwa kutumia mitandao yake ya kijamii kushiriki wimbo mpya wa Japhet Zabron, Bkakitachang’wa, pamoja na wimbo Bhamagaka wa kundi la Zabron Singers.
Akizungumza kuhusu jambo hilo, Japhet amesema kitendo hicho ni upendo mkubwa kwake na kwa kundi lake, akieleza kuwa Charlene ni mtu mwenye ushawishi katika Afrika Mashariki.
“Nimefurahia kuona wifi na shemeji wa Taifa Charlene baada ya ndoa anasikiliza wimbo Bkakitachang’wa, huu ni upendo mkubwa kwangu na kwa Zabron Singers na kwa Watanzania wote,” amesema Japhet.


