Na mwandishi wetu, Gazetini – RUVUMA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameiagiza Taasisi ya Kupambana na Rushwa [TAKUKURU] kuichunguza kampuni iliyopewa mradi wa soko la Mansese ‘A’ na ‘B’ Wilayani Songea, Ruvuma.
Wakati huo huo, amemtaka Waziri mwenye dhamana ya TAMISEMI kuchukua hatua dhidi ya uzembe katika usimamizi wa mradi huo, akisisitiza kuwa lazima viongozi wawajibike kwa dhamana walizopewa.
Akizungumza na wananchi wa Songea wakati wa ziara yake mkoani Ruvuma, Ndejembi amembana kwa maswali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Wakili Bashir Muhoja, akitaka kufahamu sababu za mkandarasi kuongezewa muda wa utekelezaji hadi Machi, 2027.
Mradi huo wa miezi 18, ambao mkataba wake ulianza mwaka 2025, ulitarajiwa kukamilika Septemba 2026 lakini umechelewa licha ya mkandarasi kulipwa Shilingi bilioni tatu kama malipo ya awali.
“Hebu tubadilike. Tuwe ‘accountable’ [wawajibikaji] na fedha za umma. ‘High-level meeting’ [vikao] inakusaidia nini?,” amehoji Ndejembi akipinga utaratibu wa viongozi kuendelea kufanya vikao vya kumbembeleza mkandarasi badala ya kumchukulia hatua.
Kwa upande mwingine, Ndejembi ametoa maelekezo kwa viongozi wanaosimamia miradi ya maendeleo kuacha kubembelezana na wakandarasi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali haiwezi kuvumilia uzembe unaosababisha wananchi kuendelea kupata kero, huku fedha nyingi za umma zikiwa zimetumika bila miradi kukamilika kwa wakati.
Makamu wa Rais anaendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Ruvuma, akitarajiwa kuelekea mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.


