Na mwandishi wetu, Gazetini
MFANYABIASHARA na Mwenyekiti wa Taifa Group, Rostam Aziz, ametoa wito wa kujenga mazingira yatakayowawezesha Watanzania, hususan vijana, kumiliki na kuongoza kampuni kubwa zinazozalisha utajiri, akisema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hayapaswi kupimwa kwa ukubwa wa uchumi pekee, bali pia ushiriki wa wananchi katika umiliki wa rasilimali na biashara.
Rostam ametoa wito huo Novemb 7, 2026 jijini Dar es Salaam alipokuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Umahiri katika Sekta za Ujenzi na Madini (African Construction and Mining Excellence Awards – ACAMEA 2026), ambako alizungumzia umuhimu wa Watanzania kuwa sehemu ya umiliki na uongozi wa kampuni zitakazochochea ukuaji wa uchumi.
Amesema anaunga mkono lengo la Tanzania la kujenga uchumi wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, lakini akasisitiza kuwa ni muhimu kujiuliza ni nani watakaomiliki kampuni, mitambo na teknolojia zitakazozalisha utajiri huo.

“Makadirio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu yanaonyesha kwamba vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 34 wataongezeka kutoka milioni 21 hivi sasa na kufikia milioni 42 mwaka 2050. Hawa ni vijana ambao tutapaswa kuwapa fursa, si fursa za ajira tu, bali nafasi ya kujenga na kumiliki biashara pia,” amesema.
Ameonya kuwa bila kujenga kampuni kubwa za Kitanzania zenye uwezo wa kuzalisha utajiri, vijana wa kizazi kijacho wanaweza kukosa nafasi ya kumiliki sehemu ya uchumi huo, licha ya kuwa ndiyo watakaokuwa sehemu kubwa ya nguvu kazi nchini.
Rostam amesema Tanzania haipaswi kuridhika kwa kuwaachia vijana miundombinu kama barabara, reli na majengo pekee, bali inapaswa pia kujenga kampuni zenye uwezo wa kuendeleza miundombinu na shughuli za kiuchumi za baadaye.
“Tusijenge uchumi wa Dola trilioni moja ambao vijana wetu watakuwa watazamaji tu. Tujenge uchumi ambao vijana hawa watakuwa washiriki, viongozi na wamiliki,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa mustakabali wa uchumi wa Tanzania hautategemea tu kiwango cha uwekezaji kitakachovutia nchini, bali pia uwezo wa Watanzania kushiriki katika kuongoza na kumiliki sehemu ya uchumi huo.


