24 C
New York

Transfoma nne zasafirishwa kwenda mradi wa Taza

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

TIMU mbili za usafirishaji wa transfoma nne kubwa zimeanza safari kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea katika vituo vya kupoza umeme vya Mradi wa TAZA, unaohusisha njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa kupitia Kisada, Mbeya na Tunduma hadi Sumbawanga.

Usafirishaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange, la kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kuchaji njia ya umeme kuelekea Sumbawanga kabla ya Novemba 15, 2026.

Timu ya kwanza inasafirisha transfoma kuelekea Kituo cha Kupoza Umeme cha Iganjo mkoani Mbeya na Kituo cha Mkangamo mkoani Songwe, huku timu ya pili ikiwa na transfoma mbili ambazo tayari zimewasili mkoani Iringa.

Meneja wa Mradi wa TAZA, Mhandisi Kelvin Mwasege, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha agizo la kukamilisha mradi linafikiwa ndani ya muda uliowekwa.

“Zoezi hili ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkurugenzi wa Tanesco, Lazaro Twange, kuhakikisha kabla ya tarehe 15 Novemba 2026 tunachaji njia yetu ya umeme inayoanzia Kituo cha Tagamenda Iringa kuelekea Sumbawanga,” amesema Mwasege.

Transfoma MVA 250 na 200

Mhandisi wa Mradi wa TAZA anayesindikiza timu ya pili, Mhandisi Esau Magori, amesema transfoma yenye uwezo wa MVA 250 itawekwa katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Iringa, huku yenye uwezo wa MVA 200 ikiwekwa katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Kisada.

“Hapa tuna transfoma mbili, ambapo yenye MVA 250 tutaifunga kwenye Kituo cha Kupoza Umeme cha Iringa na ya MVA 200 tutaifunga Kituo cha Kupoza Umeme cha Kisada,” amesema Magori.

Amesema kukamilika kwa Mradi wa TAZA kutaiunganisha Rukwa kwenye Gridi ya Taifa, pamoja na kuweka mazingira ya kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia kwa ajili ya biashara ya umeme.

“Umuhimu wa huu mradi utasaidia kuunganisha Mkoa wa Rukwa kwenye Gridi ya Taifa na zaidi ya yote utakwenda kuiunganisha Tanzania na Zambia katika biashara ya kuuziana umeme,” amesema.

Twange alitoa agizo la kukamilisha Mradi wa TAZA ifikapo Novemba 15, 2026, alipokutana na wakandarasi na wasimamizi wa mradi huo mkoani Iringa.

Related articles

Recent articles