LOS ANGELES, Marekani
TANGU Bill Clinton alipomaliza majukumu yake ya urais wa Marekani mwaka 2001, amekuwa akiishi Chappaqua, New York, makazi yaliyozungukwa na miti, na kama haitoshi, ni mbali na kamera na macho ya umma ili kupata muda mwingi wa kupumzika.
Ni makazi ya gharama na amekuwa akiishi hapo pamoja na mkewe, Hillarry Clinton. Nyumba aliyoinunua mwaka 1999, ambapo vyanzo vya habari vinaeleza kuwa aliinunua kwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 1.7.
Ni mjengo wa vyumba 11 na ameendelea kuishi hadi leo. “Tunavutiwa nayo. Ni nzuri, tunaipenda sana,” alisema Clinton.
Kwa upande mwingine, Clinton na Hillarry wanafahamika kwa mapenzi yao ya nyumba nzuri. Kama itakumbukwa, mwaka 2000, wanandoa hao walitumia Dola milioni 2.85 kununua nyumba yenye vyumba vine vya kulala. Ni nyumba ambayo Hillarry aliitumia kuandika kitabu chake cha ‘Hard Choices’.
Mwaka 2016, waliongeza nyumba nyingine jijini New York, ambayo iliwagharimu Dola milioni 1.16, ikiwa na ukubwa wa futi za mraba 3,600, vyumba vitatu vya kulala, bwawa la kuogelea, kuta zilizonakshiwa kwa mawe, na miti inayolifanya eneo hilo liwe na hewa safi.
Pia, historia inaturudisha mwaka 1980, ambapo baada ya kukosa muhula wa pili wa nafasi ya gavana, Clinton na mkewe walinunua nyumba yenye thamani ya Dola 112,000.
Miaka mitano kabla ya hiyo, walishanunua nyumba ya chumba kimoja mjini Arkansas, ambayo iliwagharimu Dola 17,200. Ni nyumba ambayo walinunua miezi michache tu kabla ya kufunga ndoa.
Wakati huo, tayari walishakuwa na nyumba nyingine ya vyumba viwili vya kulala, ambayo waliinunua mwaka 1977 kwa Dola 35,000, wakati huo Clinton akiwa na umri wa miaka 31 tu. Mwaka uliofuata, ndipo akachaguliwa kuwa gavana.


