22.3 C
New York

Usiyoyajua kuhusu mauaji ya halaiki ya Rwanda 1994 (3)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

UHASAMA mkubwa wa jamii ya Wahutu na Watutsi ulishuhudiwa tena mwaka 1990. Ni baada ya kundi la Rwandan Patriotic Front (RPF) kutoka Uganda kuivamia Rwanda. Ni kundi la waasi likiongozwa na Watutsi.

Inaelezwa kuwa mashambulizi ya risasi kati ya RPF na wanajeshi wa Serikali ya Wahutu chini ya Rais Juvenal Habyarimana yalishuhudiwa mwanzoni mwa mwaka 1991.

Baadaye, pande mbili hizo, kwa maana ya RPF na Serikali ya Habyarimana, ambaye anatokea kabila la Wahutu, zilikaa chini mwaka 1992, ajenda ikiwa ni kusaka suluhu ya mgogoro.

Makubaliano yaliyofikiwa na kusainiwa Agosti, 1003, ni pamoja na kuundwa kwa serikali ya mpito, ambayo ingewahusisha pia wawakilishi kutoka kundi la RPF, jambo ambalo Wahutu wengi hawakukubaliana nalo.

Kampeni zilizobeba ajenda ya kuwapinga Watutsi zilianza mara moja, zikipewa nafasi kubwa kupitia vyombo vya habari, hasa magazeti na vituo vya redio nchini Rwanda.

Upepo ulibadilika na kuwa mbaya zaidi usiku wa Aprili 6, 1994, baada ya ndege iliyokuwa imembeba Rais Habyarimana na Rais wa Burundi, Cyprien Ntaryamira, kudunguliwa mjini Kigali. Kila aliyekuwa kwenye ndege alipoteza maisha.

Licha ya kwamba haikufahamika ni nani au kundi gani lilitekeleza shambulizi hilo, Wahutu walibebeshwa lawama, kwamba ndiyo walioiangusha ndege hiyo. Baadaye, ikaelezwa pia kwamba ni RPF.

Kuanzia usiku huo, Wahutu walianza msako wa kuwatafuta, kuwapiga na kuwaua Watutsi. Waziri Mkuu, Agathe Uwilingiyimana, ambaye pia alikuwa anatokea kabila la Wahutu, aliuawa siku iliyofuata. Walinzi wake 10 raia wa Ubelgiji nao waliuawa katika tukio hilo.

Taarifa zinaeleza kuwa kuuawa kwa Uwilingiyimana ulikuwa ni mpango wa kuondosha viongozi wa makabila yote mawili (Wahutu na Watutsi) ili Kanali wa jeshi, Theoneste Bagosora, achukue nchi.

Siku mbili baadaye, kwa maana ya Aprili 8, 1994, Spika wa Bunge, Theodore Sindikubwabo, alitangazwa kuwa Rais wa Mpito, kabla ya kuapishwa siku iliyofuata.

Usikoe sehemu ya nne ya makala haya … Tembelea www.gazetini.co.tz

Related articles

Recent articles