22.1 C
New York

Usiyoyajua kuhusu mauaji ya halaiki ya Rwanda 1994 (4)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA sehemu ya tatu ya makala haya, tuliona kilichotokea Aprili 8, 1994, ambapo Spika wa Bunge, Theodore Sindikubwabo, alitangazwa kuwa Rais wa Mpito, kabla ya kuapishwa siku iliyofuata. Endelea …

Miezi michache iliyofuata, vikundi vya Wahutu, ‘Interahamwe’ na ‘Impuzamugambi’ viliendelea na operesheni ya kuua watu wa jamii ya Watusti na mbaya zaidi vyombo vya habari navyo vilijikuta kwenye mtego wa kueneza chuki.

Matangazo ya redio yalihamasisha mauaji dhidi ya Watutsi, ambao wakati huo walibezwa na kudhalilishwa kwa kupachikwa jina la ‘cockroaches’, kwa maana ya ‘mende’ kwenye lugha ya Kiswahili.

Zipo taarifa kuwa baadhi ya viongozi wa jeshi na vikundi vyenye silaha walilazimisha wananchi wa jamii ya Wahutu kujiingiza pasi na matakwa yao kwenye mauaji dhidi ya Watutsi.

Matukio ya Watutsi kuuawa kwa kupigwa mapanga, kubakwa na kuambukizwa magonjwa ya zinaa, ukiwamo Ukimwi, yalishamiri dhidi ya wanawake wa jamii hiyo.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Mpango Maalumu wa Kuisaidia Rwanda (UNAMIR), waliingilia na kutuliza kwa kiasi fulani hali mbaya iliyokuwepo awali.

Julai 19, 1994, iliundwa Serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa, ambayo ingezingatia mgawanyo wa madaraka usiotokana na kabila moja, bali kutoa fursa sawa kwa pande zote (Wahutu na Watutsi).

Katika Serikali hiyo, Pasteur Bizimungu wa kabila la Wahutu akateuliwa kuwa Rais, huku kiongozi wa Kundi la RPF, Paul Kagame, ambaye ni Mtutsi akawa Makamu wa Rais. Huo ukawa mwisho wa mauaji ya halaiki.

Licha ya kwamba Wahutu bado walikuwa wengi serikalini, zilikuwepo jitihada za kuondosha tofauti. Moja ya hatua hizo ikawa ni kubadili baadhi ya nembo, ikiwamo bendera na wimbo wa Taifa, ambavyo vyote vilibeba sura na mwelekeo wa jamii ya Wahutu.

Katiba Mpya ya mwaka 2003 ikafuatiwa na Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa kidemokrasia tangu Rwanda ilipopata uhuru. Kagame aliyekuwa ameshikilia kiti baada ya Rais Bizimungu kujiuzulu mwaka 2000, akachaguliwa na amebaki hapo hadi leo hii (2026).

Kwa upande mwingine, hata baada ya kumalizika kwa vita hivyo, washukiwa wa mauaji waliendelea kutafutwa na kufunguliwa mashitaka na wengine walikumbana na hukumu zao, ikiwamo kifungo cha maisha gerezani.

Miongoni mwa waliowahi kuangukiwa hukumu ni aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Jean Kambanda, ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha Septemba 4, 1998. Alijaribu kukata rufaa mwaka 2000 lakini ilitupiliwa mbali.

Wengine ni waliokuwa makamanda wa jeshi, Anatole Nsengiyumva na Aloys Ntabakuze, pamoja na aliyekuwa ‘bosi’ wao, Gratien Kabiligi, ambao kila mmoja alihukumiwa kifungo cha maisha Desemba 18, 2008.

Baadaye, Kabiligi alifutiwa hukumu, wakati Bagosora alipunguziwa hadi miaka 35 gerezani, kama ilivyokuwa kwa Nsengiyumva aliyepunguziwa hadi miaka 15, kisha kuachiwa.

NB: Hii ni sehemu ya mwisho ya makala haya ya ‘Usiyoyajua kuhusu mauaji ya halaiki ya Rwanda 1994’. Kama ulipitwa na sehemu zilizopita, tembelea www.gazetini.co.tz.

Related articles

Recent articles