24 C
New York

Tanesco kutumia bilioni 63.19 kujenga njia ya umeme Mpomvu–GGM

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SERIKALI kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Mpomvu hadi Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha GGM, Geita, wenye urefu wa takribani kilomita 6.7.

Mradi huo utakaogharimu Sh bilioni 63.19 unalenga kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme kwa GGM, huku ukitarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea uzalishaji, ajira, mapato na uwekezaji katika eneo hilo.

Akizungumza Septemba 3, 2026, jijini Dodoma, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya umeme ili iendane na kasi ya ukuaji wa mahitaji.

“Serikali itaendelea kushirikiana na Tanesco na wadau wote wa sekta ya nishati kuhakikisha miundombinu ya umeme inaendana na kasi ya ukuaji wa mahitaji. Tunataka kuona umeme unaozalishwa nchini ukitumika kikamilifu kuchochea uzalishaji, kuongeza ajira, kuongeza mapato na kuvutia uwekezaji zaidi. Mradi huu ni kielelezo cha falsafa hiyo,” amesema Makamba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, amesema mradi huo utatekelezwa ndani ya miezi 18 kuanzia tarehe ya kusaini mkataba, huku akieleza kuwa GGM ni miongoni mwa wateja wakubwa wa Shirika na wanaochangia kwa kiasi kikubwa katika mapato yake.

“Mradi huu unagharimu takribani Shilingi bilioni 63.19 za Kitanzania na kutokana na kuwa GGM ni miongoni mwa wateja wetu wakubwa wenye kuchangia kiasi kikubwa cha mapato kwa Shirika, tutahakikisha mradi huu unafanikiwa kama inavyotarajiwa kukidhi ongezeko la mahitaji yao kwa manufaa ya pande zote mbili na pato la Taifa kwa ujumla,” amesema Twange.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Balozi Zuhura Bundala, amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uwezo wa Shirika kukidhi mahitaji ya wateja, huku ukifungua fursa zaidi za uwekezaji na ajira.

“Utiaji saini huu ni sehemu ya kimkakati kujenga uwezo wa Tanesco kukidhi mahitaji ya wateja na kufungua fursa za uwekezaji na ajira. Bodi tutaendelea kuisimamia Tanesco kukidhi ongezeko la hitaji la umeme kwa kuimarisha na kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya umeme,” amesema Bundala.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, ameipongeza Bodi ya Tanesco kwa usimamizi wa Shirika katika kuunga mkono ujenzi wa uchumi wa kisasa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Subira Mgalu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashimu Komba, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, amesema Serikali ya Mkoa imejipanga kushirikiana na mkandarasi kuhakikisha mradi huo unatekelezwa bila vikwazo.

“Ni dhahiri, nishati ya umeme inachagiza maendeleo ya sekta zote. Tunampongeza Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anavyosukuma kwa dhati agenda ya nishati ya umeme kuwafikia wananchi. Mamlaka ya Mkoa imejipanga kushirikiana na Mkandarasi wa mradi wa umeme wa Mpomvu–GGM kuhakikisha mradi haupati kikwazo,” amesema Komba.

Kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha GGM kuacha kutegemea njia ya awali ya msongo wa kilovoti 33 iliyokuwa ikipeleka umeme katika eneo hilo. Aidha, mradi unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika Geita na maeneo ya pembezoni, kuongeza ufanisi wa shughuli za uzalishaji na kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji mpya.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuongeza uwezo wa mfumo wa usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo.

Related articles

Recent articles