22.2 C
New York

Safari ya Ndejembi kurithi mikoba ya Dk. Nchimbi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

HATIMAYE kiatu cha Dk. Emmanuel Nchimbi katika nafasi ya Makamu wa Rais kimevaliwa na Deogratius John Ndejembi. Ni uamuzi uliotangazwa jana Agosti 26, 2026 na Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ndejembi (43), atakuwa Makamu wa Rais wa 13 tangu Tanzania ilipopata uhuru wake kutoka kwa Serikali ya ukoloni ya Uingereza mwaka 1961.

Kwa wanaofuatilia siasa za Tanzania, Ndejembi si jina geni, ingawa ni umaarufu wake ni wa wastani, ikilinganishwa na walionao wanasiasa wengi ndani ya CCM na Serikali kwa ujumla. Amekuwa Waziri wa Nishati tangu mwaka 2025 na amekuwa kwenye siasa na utumishi wa umma kwa miaka zaidi ya 10.

ELIMU YAKE

Ndejembi alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi ya Cannon Andrea Mwaka, alikosoma kati ya mwaka 1988 na 1995. Aliendelea na Sekondari ya Kigurunyembe (1996 – 1998), kabla ya kwenda Merton College (2002 – 2004).

Kati ya mwaka 2006 na 2009, alisoma Shahada ya Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Lincoln nchini Uingereza. Kati ya mwaka 2009 na 2012, alisoma Stashahada ya Juu katika Taasisi ya Usimamizi wa Utawala.

SEKTA BINAFSI, CCM HADI SERIKALINI

Safari yake ilianzia katika sekta binafsi, ambapo mwaka 2012 alikuwa meneja wa Kampuni ya A1 Outdoor, kabla ya kuwa Mkuu wa Mauzo katika Kampuni ya Smile Communication (2012 – 2014).

Mwaka 2014, aliajiriwa na Tigo (sasa Yas) kushika nafasi ya Meneja wa Kanda, akihudumu hapo hadi mwaka 2015. Mwaka uliofuata, alihamia GSM Group na kuwa Mkuu wa Idara ya Masoko.

Safari ya Ndejembi ndani ya CCM ilianzia mbali, tangu akiwa kijana, ambapo alikuwa mwanachama wa Baraza la Taifa la Umoja wa Vijana wa CCM (2008 – 2017). Kwa upande mwingine, aliwahi kuwa mwanachama wa Baraza Kuu la CCM, kisha kuhamia Kamati yake ya Siasa.

Ni hadi mwaka 2016, ndipo alipoingia katika utumishi wa umma baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dodoma. Alishika nafasi hiyo hadi mwaka 2020.

Miaka minne baadaye, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Chamwino, Dodoma, kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri. Kuanzia mwaka 2021 hadi 2023, alikuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kisha kuhamia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mwaka 2024, alipandishwa na kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na mwaka huo pia alihamishiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambako alihudumu kama Waziri hadi mwaka 2025.

Ni baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ndipo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipomteua kuwa Waziri wa Nishati, akishughulika na uzalishaji na usambazaji wa umeme na sekta za mafuta na gesi.

Related articles

Recent articles