ZEIST, Uholanzi
KIUNGO na kocha wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez, ndiye aliyekabidhiwa benchi la ufundi kwa ajili ya kuinoa timu ya soka ya Taifa ya Uholanzi ‘Oranje’.
Xavi ana historia ndefu na Waholanzi. Kocha wa zamani wa Uholanzi, Louis van Gaal, ndiye aliyeibua kipaji chake kwa kumpa nafasi katika kikosi cha Barcelona.
Akiwa mchezaji muhimu wa Barcelona baadaye, Xavi alitwaa mataji 25, yakiwamo manne ya Ligi ya Mabingwa na nane ya Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).
Kwa miaka minne aliyocheza timu ya Taifa, aliiwezesha Hispania kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2010, ambapo waliifunga Uholanzi katika mechi ya fainali, na EURO (2008 na 2012).
Pia, staili ya uchezaji wa pasi nyingi iliyoipa mafanikio makubwa Barcelona iliasisiwa na gwiji la soka la Uholanzi, Johan Cruyff, wakati huo akiwa kocha katika miaka ya 1970.
Xavi (46), amekuwa nje ya kazi ya ukocha tangu alipoachana na Barcelona mwaka 2024 na amepewa kibarua cha kuvaa viatu vya Ronald Koeman aliyeondoka kwenye benchi baada ya kuishia hatua ya 32 Bora ya fainali zilizopita za Kombe la Dunia.
KAZI ALIYOIKATAA GUARDIOLA
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Soka la Uholanzi, Nigel de Jong, amesema Xavi alikuwa miongoni mwa makocha wanne waliokuwa kwenye rada zao.
Pep Guardiola na Arne Slot, ambao wote hawana ajira baada ya kuondoka Manchester City na Liverpool, walikataa ofa yao. Mwingine ni kocha wa sasa wa timu ya vijana ya Uholanzi, Michael Reiziger.
Uholanzi, licha ya kuzalisha vipaji vingi vya soka katika historia ya soka, haijawahi kutwaa Kombe la Dunia. Imefika fainali mara tatu na kupoteza zote.
ANA KWA ANA NA KLOPP
Xavi akiwa kocha mpya, ataanza kuisimamia Uholanzi katika mechi ya mashindano ifikapo Septemba 24, 2026, ambapo watakuwa nyumbani mjini Amsterdam kumenyana na wababe Ujerumani.
Ujerumani ambayo kwa sasa iko chini ya kocha mpya, Jurgen Klopp, ambaye amechukua nafasi ya Julian Nagelsmann aliyeachia ngazi baada ya fainali zilizopita za Kombe la Dunia.
Akizungumzia kukutana na Ujerumani, Xavi amesema: “Najisikia vizuri. Nafurahia kwa sababu tunakutana na timu kubwa Ulaya na yenye kocha bora kwa miaka ya hivi karibuni, Jurgen Klopp.”


