MADRID, Hispania
MWANASOKA raia wa Argentina anayecheza eneo la ushambuliaji, Julian Alvarez, alijiunga na Atletico Madrid mwaka 2024 akitokea Manchester City na usajili wake uligharimu kitita cha Pauni milioni 81.
Kwa miaka miwili aliyocheza Man City iliyomsajili kwa Pauni milioni 14.1 akitokea River Plate ya Argentina, alifunga mabao 36 katika mechi 106 na kutwaa mataji sita, yakiwamo matatu kwa mpigo mwaka 2023 (Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Ulaya na FA Cup).
Akiwa Atletico Madrid anayoitumikia kwa sasa, Alvarez amefunga mabao 49 katika mechi 107 lakini uhusiano wake na mashabiki wa klabu hiyo umeonekana kuyumba katika siku za hivi karibuni.
Wikiendi iliyopita, wakati Atletico Madrid wakilazimishwa sare ya mabao 2-2 na Villarreal, mashabiki walimzomea na hiyo inachochea mpango wa kuondoka kabla ya dirisha la usajili kufungwa Septemba 1, 2026.
Alvarez mwenye umri wa miaka 26, anataka kutimkia Barcelona ambayo nayo inamuhitaji. Kwa kuishi Catalunya, anaona itakuwa rahisi kuwa karibu na familia yake.
Hata hivyo, biashara kati ya Atletico na Barcelona inakuwa ngumu kutokana na ukweli kwamba klabu hiyo ya jijini Madrid haiko tayari kuwauzia silaha wapinzani wao hao wa La Liga.
Kwa upande mwingine, Arsenal wako mlangoni wakati wote. Baada ya kumkosa Vinicius Jr aliyeamua kubaki Madrid, kocha Mikel Arteta ameelekeza nguvu kwa Alvarez.
Lakini sasa, Alvarez, kwa upande wake, anaona kuishi Uingereza kutaipa wakati mgumu familia yake. Ili kumtembelea italazimika kufuata taratibu za viza, tofauti na wanavyoishi pamoja nchini Hispania.
Hivi karibuni, ziliibuka taarifa kuwa Mkurugenzi wa Atletico Madrid, Mateu Alemany, alikuwa jijini London na kukutana na wawakilishi wa Arsenal, ambapo aliwaambia Alvarez anapatikana kwa dau la Pauni milioni 128.


