TEHRAN, Iran
KATIBU Mkuu wa Hazina ya Marekani, Scott Bessent, amesema si tu Iran, bali hata nchi, taasisi na mashirika yatakayofanya biashara na Iran yataingia kwenye vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa nchi hiyo.
Akizungumza hivi karibuni, Agosti 24, 2026, Bessent alisema Marekani imelenga sekta nyeti, ikiamini kwa kuzikaba hizo, basi uchumi wa Iran utaanguka moja kwa moja.
Katika hotuba yake, alisema Marekani imelenga maeneo muhimu yanayoipa jeuri ya kiuchumi nchi hiyo ya Kiarabu. Maeneo hayo ni hazina za kidijitali, teknolojia, dhahabu, usafiri wa anga na meli.
“Taasi yoyote itakayosaidia utakatishaji fedha kwa ajili ya Iran itaondoshwa moja kwa moja kwenye mfumo wa kifedha wa Dola ya Marekani,” alisema na Bessent na kuongeza: “Hatua zinaanza sasa hivi.”
Aidha, hatua hiyo inatazamiwa kuiumiza Iran. Kwa miaka mingi ya kuwekewa vikwazo, Iran imekuwa ikitegemea mitandao ya nje kuwezesha mfumo wa kibenki kwa fedha zake.
Hivyo, katazo jipya linakuja wakati tayari usafirishaji wa mafuta ya Iran kwenda kwa wateja wake wakubwa, China, ukiwa umeshuka kutoka mapipa milioni 1.58 kwa siku hadi 823,000 na sasa 534,000.
Takwimu zinaonesha kuwa bei ya vyakula imepanda kwa asilimia 128, huku thamani ya sarafu ya Iran nayo ikishuka baada ya miamala mingi, ikiwamo ya uuzaji wa magari, ikifanyika kwa Dola ya Marekani.


