28.2 C
New York

Tanzania yavutia Sh trilioni 9 za uwekezaji madini ndani ya miaka minne

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SEKTA ya Madini nchini Tanzania imevutia uwekezaji wenye thamani ya Sh trilioni 9 ndani ya kipindi cha miaka minne, hatua ambayo Serikali inasema imeendelea kuiimarisha Tanzania kama miongoni mwa vivutio muhimu vya uwekezaji wa madini barani Afrika.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema hayo leo, Agosti 15, 2026, mkoani Morogoro wakati wa hafla ya utiaji saini Mikataba ya Ubia wa Uchimbaji wa Madini ya Kinywe kati ya Serikali na Kampuni ya Henan Yudi Mining.

Mavunde amesema hadi sasa Serikali imesaini jumla ya Mikataba ya Msingi 14, akieleza kuwa hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta ya madini nchini.

Akizungumzia mradi wa Kinywe, amesema una mashapo yaliyothibitishwa yanayokadiriwa kufikia tani milioni 104.28 na unatarajiwa kuwekeza takribani Dola za Marekani milioni 100, sawa na Sh bilioni 265.

Amesema mradi huo ukifikia uzalishaji wa kiwango kamili unalenga kuzalisha tani 50,000 za Kinywe kwa mwaka, huku kituo cha uchakataji kikiwa na uwezo wa kuchakata hadi tani milioni moja kwa mwaka. Aidha, zaidi ya Watanzania 600 wanatarajiwa kupata ajira za moja kwa moja.

“Serikali inaendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya madini kutoka kuwa mwenyeji wa shughuli za uchimbaji hadi kuwa mshiriki wa thamani inayozalishwa,” amesema Mavunde, akibainisha kuwa Serikali inamiliki asilimia 17 ya hisa katika mradi huo.

Amesema Kinywe ni miongoni mwa madini muhimu yanayotumika katika teknolojia za kisasa, ikiwemo utengenezaji wa anode za betri, hivyo mradi huo una nafasi ya kuiwezesha Tanzania kushiriki zaidi katika mnyororo wa thamani wa Kinywe duniani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema mradi huo utafungua fursa mpya za kiuchumi na ajira, kuongeza uzalishaji wa madini na kuchochea maendeleo ya sekta ya madini pamoja na uchumi wa Taifa.

Naye Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amezipongeza pande zote zilizoshiriki katika majadiliano yaliyowezesha kufikiwa kwa makubaliano hayo, akisema uwekezaji huo utaongeza shughuli za kibiashara, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China.

Balozi Chen amesema China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uwekezaji wa moja kwa moja nchini Tanzania, huku akieleza kuwa mradi huo unaongeza eneo jipya la ushirikiano wa kibiashara na kufungua fursa za ajira na maendeleo kwa wananchi wa eneo la mradi na Taifa kwa ujumla.

Related articles

Recent articles